Wanne washikiliwa na polisi Dar kwa unyang’anyi wa kutumia silaha

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro.

Muktasari:

  • Waliofanya uhalifu Goba wanaswa Mabibo na kubainika kuhusika na matukio mengine kadhaa ya unyang’anyi kwa kutumia silaha yaliyotokea mwanzoni mwa mwaka 2023.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam limewakamata watu wanne wanaotuhumiwa kuhusika na matukio ya unyang’anyi kwa kutumia silaha ambayo yalianza kuripotiwa mwanzoni mwa mwaka huu.

Watuhumiwa hao wakiwemo wawili ambao wamelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kufuatia majibizano ya risasi na polisi, walikamatwa wakiwa na bunduki aina ya AK47 yenye risasi 24 pamoja na bastola moja.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumatatu Januari 9, 2022, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema walipata taarifa za kundi hilo ambalo tayari limefanya matukio katika maeneo ya Kariakoo, Kunduchi Mtongani, Goba na Madale.

“Tulipata taarifa fiche kuhusu kundi hili na jana saa sita na nusu katika eneo la Mabibo External, tulifanikiwa kuwazingira na walipogundua hilo wakaanza kufyatua risasi.

“Polisi walijihami na kuwajeruhi wawili kati yao ambao hali zao ni mbaya wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Baada ya mahojiano walikiri kuhusika katika matukio hayo na ilibainika silaha walizokutwa nazo ndiyo hizo hizo zimetumika kwenye matukio yote,” amesema Muliro.