Wanunuzi lawamani huduma mbovu za afya Rukwa

Muktasari:

  • Usimamizi mbovu wa makusanyo umetajwa kuwa sababu ya kukosekana kwa dawa na vifaa tiba kwenye baadhi ya Hospitali, vituo vya afya na zahanati mkoani Rukwa.  

Sumbawanga. Usimamizi mbovu wa makusanyo yatokanayo na huduma za afya na kukithiri kwa madeni ya washitiri (wanunuzi) imetajwa ni miongoni mwa sababu za wananchi kukosa huduma bora katika hospitali na vituo vya afya mkoani Rukwa.

Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Rukwa, Samson Hango amesema hayo leo Machi 21, 2023 wakati akifungua mafunzo ya wawezeshaji mfumo wa mshitiri kwa watendaji na wataalamu wa afya mkoani humo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa RDC mjini hapa.

Hango ambaye ni Ofisa Elimu Mkoa wa Rukwa amesema kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kukosekana kwa dawa na vifaa tiba kwenye baadhi ya Hospitali, vituo vya afya na zahanati lakini hali hiyo inasababishwa na usimamizi mbovu wa makusanyo.

Amewataka wakurugenzi wa halmashauri kusimamia kikamilifu afua mbalimbali za mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya ikiwemo kufanya ukaguzi wa kitabibu mara kwa mara kwenye vituo vinavyotoa huduma za afya ili kupunguza changamoto zinazotokana na usimamizi mbovu wa bidhaa hizo.

"Huu mfumo tunaokwenda kuutekeleza uwe chachu ya kuboresha huduma zetu za afya katika halmashauri zetu, tusimamie vizuri mapato ya huduma za afya, tukifanikiwa hilo tutaweza kuwalipa washitiri kwa wakati hivyo kutoa huduma bora na kuondoa malalamiko yote ya wananchi," amesisitiza.

Awali, Mwakilishi wa Tamisemi katika mafunzo hayo, Hamimu Abdallah amesema mfumo huo wa kieletroniki utaondoa urasimu katika upatikanaji wa dawa kwa uhakika kati ya watoa huduma na Washitiri hivyo kusaidia kuondoa changamoto kukosekana kwa wakati kwa dawa na vipimo kwenye vituo vinavyotoa huduma za afya.


Ameongeza kwamba mfumo unawezesha upatikanaji wa bidhaa za afya zinazokuwa zimekosekana bohari ya dawa (MSD) hivyo kurahisisha na kuimairisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwenye vituo hivyo na kupunguza hoja za kiukaguzi kwenye ununuzi wa bidhaa hizo hapa nchini.