Waratibu Elimu ya Afya mikoa 26 wajengewa uwezo

ARUSHA. Waratibu elimu ya afya kwa umma kutoka mikoa 26 Tanzania Bara wamejengewa uwezo katika kudhibiti wingi wa taarifa na kuepuka upotoshaji unaoweza kujitokeza katika jamii wakati kuna magonjwa ya milipuko.

Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkurugenzi msaidizi sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, wizara ya Afya, Dk Tumaini Haonga wakati akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku mbili.

Amesema wanataka kuhakikisha taarifa inayotolewa kwa umma kuhusu magonjwa ya milipuko lazima iwe taarifa sahihi kwani kumekuwepo na wingi wa taarifa zinazosahihi ambazo zimekuwa zikitolewa na kusababisha taharuki kwa wananchi.

Aidha ameongeza lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha wanakuwa wepesi kutoa taarifa sahihi kwa wananchi na kutoa elimu ya afya kuhusu kinga na tahadhari ndo maana wameamua kuchukua wataribu kutoka mikoa yote ambao watasimamia maswala hayo kwa karibu zaidi.

"Wakati wa kuwepo wa magonjwa hayo ya milipuko kumekuwepo kwa wingi wa taarifa huku baadhi zikiwa na ukweli nyingine zikiwa hazina ukweli ambapo mafunzo hayo yataelekeza waratibu kuzingatia utoaji wa  elimu, na ujumbe kwa kuzingatia miongozo ya Wizara ya Afya," amesema Dk Tumaini.

Mtaalamu wa Elimu ya Afya kwa Umma WHO Tanzania, Dk Neema Kileo amesema mafunzo hayo yameandaliwa na wizara ya afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) na  Mtandao unaojishughulisha na Udhibiti wa milipuko ya taarifa Afrika (AIRA)ambapo mafunzo kama hayo yameshafanyika  Zanzibar.

Dk Kileo amesema mafunzo hayo yamewashirikisha wadau mbalimbali kutoka mashirika ya UNICEF, USAID, CDC, TRCS, John Hoplains University, Shirika la Save the Children, na AMREF Health Africa.

'Tumefikia  hatua ya kutoa mafunzo hayo baada ya kuona kuna changamoto ya utoaji wa taarifa hasa wakati wa magonjwa ya milipuko na kuleta taharuki kubwa kwenye jamii na hivyo kusababisha watu kushindwa kujua ni watu gani sahihi wa kuwasikiliza na hivyo kushindwa kujua ni hatua gani sahihi  za kuchukua" amesema Kileo

Ameongeza lengo kubwa ni kuhakikisha wanakuwa na wataalamu nchi nzima wenye uwezo wa kukabiliana na mlipuko  wa taarifa na mwisho kupata taarifa zilizo sahihi na kujua cha kufanya haraka  kwani  ukitaka  kudhibiti lazima uwe na taarifa sahihi.

Mmoja wa washiriki, Mratibu wa elimu ya afya kwa umma kutoka mkoa wa Tanga, John Sagaika amesema kupitia mafunzo hayo ya ufuatiliaji taarifa magonjwa ya milipuko ngazi ya jamii itawasaidia sana katika utendaji kazi wao katika kujikinga  na magonjwa ya milipuko  kwa kutoa taarifa na elimu iliyo sahihi kwa wananchi.