Wasafirishaji Kanda ya Ziwa wapinga gharama za ukaguzi

Mkurugenzi wa Huduma za Usafiri Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (uchukuzi), Aron Kisaka akisisitiza jambo wakati wa mkutano wa wadau wa usafirishaji Kanda ya Ziwa jijini Mwanza. Picha na Damian Masyenene

Muktasari:

Kwa mujibu wa rasimu za kanuni mpya za Latra za mwaka 2023, ada za ukaguzi zinazopendekezwa ni Sh90, 000 kwa magari ya abiria kuanzia watu 61 na kuendelea, Sh70, 000 kwa gari yanayopakia abiria 46 hadi 60 na Sh50, 000 kwa mabasi yanayobeba abiria 24 hadi 45.

Mwanza. Vyama vya Wasafirishaji wa Abiria Kanda ya Ziwa wamepinga mapendekezo ya bei mpya za ukaguzi wa magari zinazotajwa kwenye rasimu za kanuni mpya za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra).

Wakizungumza jijini Mwanza Mei 17, 2023 wakati wa mkutano wa kupokea maoni ya wadau uliohudhuriwa na wawakilishi kutoka vyama vya wamiliki wa mabasi, wamiliki na madereva wa daladala, maguta, bajaji, magari ya mizigo wamependekeza bei ya sasa ya Sh5,000 ndiyo  iendelee kutozwa.

Kwa mujibu wa rasimu za kanuni mpya za Latra za mwaka 2023, ada za ukaguzi zinazopendekezwa ni Sh90, 000 kwa magari ya abiria kuanzia watu 61 na kuendelea, Sh70, 000 kwa gari yanayopakia abiria 46 hadi 60 na Sh50, 000 kwa mabasi yanayobeba abiria 24 hadi 45.

Kanuni hizo zinapendekeza ada ya ukaguzi kwa magari yanayopakia abiria 16 hadi 25 iwe Sh30, 000, wakati ada ya Sh20, 000 inapendekezwa kwa magari ya abiria abiria 4 hadi 15 huku pikipiki za magurudumu matatu maarufu kama bajaji ikipendekezwa zitozwe Sh15, 000 na pikipiki za magurudumu mawili yanatakiwa zilipe Sh10, 000.

Katibu wa Wamiliki wa Mabasi (Taboa) Kanda ya Ziwa, Anuary Said amesema mapendekezo ya bei mpya na takwa la ukaguzi wa magari kufanyika mara mbili kwa mwaka utaongeza siyo tu gharama za usafirishaji kwa wamiliki, bali pia itaathiri abiria ambao ndio watabeba gharama hizo.

Katika mapendekezo ya Taboa Kanda ya Ziwa, kazi ya kukagua vyombo vya usafirishaji, hasa mabasi makubwa inatakiwa kufanywa na taasisi moja yenye uwezo itakayoteuliwa na Serikali badala ya shughuli hiyo kuhusisha taasisi tofauti, hali inayoongeza usumbufu kwa wamiliki.

"Latra na mamlaka nyingine za Serikali zijiridhishe na uwezo wa kiutendaji wa taasisi za ukaguzi na kuziorodhesha ili zijulikane kwa wadau badala ya kutegemea Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT)," amesema Anuary

Mwenyekiti Chama cha Wasafirishaji Abiria Mkoa wa Mwanza, Yusuph Lukinja amesema bei zinazopendekezwa hazijazingatia hali halisi katika sekta ya usafirishaji huku akishauri jukumu la ukaguzi wa vyombo vya usafirishaji likabidhiwe kwa Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani.

Katibu Mkuu wa Victoria Driving Association, Mwaka Samson ameshauri vyombo vya usafirishaji vinavyoingizwa nchini vikiwa tayari vimetumika katika mataifa mengine yaondolewe katika mfumo mpya wa ukaguzi unaopendekezwa.

Akijibu baadhi ya hoja za wadau, Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabarani kutoka Latra, Johansen Kahatano amewatoa hofu kuhusu mfumo mpya akisema utatumia mitambo ya kisasa na tayari mchakato wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi kuhusu uwekezaji katika mfumo huo.

"Mchakato ukikamiliki, vituo vya ukaguzi wa magari vitajengwa maeneo mbalimbali nchini na Jeshi la Polisi ni kati ya wadau muhimu watakaotekeleza jukumu la ukaguzi wa magari mara mbili kwa mwaka,’’ amesema Kahatano

Mkurugenzi wa Huduma za Usafiri Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (uchukuzi), Aron Kisaka amewaomba wadau wa sekta ya usafirishaji kuendelea kutoa maoni yao kuhusu kanuni hizo hadi Mei 30, mwaka huu, huku akiahidi kuwa maoni na mapendekezo yao yatazingatiwa kufikia maamuzi ya mwisho.

"Maoni yote ya wadau kutoka kanda zote yatajumuishwa kuboresha mapendekezo ya kanuni hizi; lengo ni kulinda wataoa huduma, abiria na kila anayeguswa na huduma za usafirishaji bila kuathiri ubora na mapato ya Serikali," amesema Kisaka.