Wasanii wetu na vifo vya ajali

Tuesday July 26 2022
VIFO PIC
By Dk Levy

Maunda Zorro, sauti tamu kutoka kwenye uso wenye macho matamu, imebaki historia. Mwili umezingirwa na udongo ndani ya kaburi. Hatunaye kinafsi na kimwili pia. Mungu amuepushe na adhabu ya kaburi. Hii inaumiza sana.

Pole kwa Mzee Zorro, kwa Banana, na uzao wa Maunda, na ni maumivu kwa familia ya Bongo Fleva pamoja na wapenzi wote wa muziki wa kizazi kipya. Hakuondoka binadamu tu, bali mtoto wa kike na sauti yake tamu imetuacha.

Ni wapi tutaipata sauti hii tena? Hapana! Kifo ni katili zaidi ya ukatili kwa maisha ya wanadamu. Ukatili wa kifo hukolea zaidi pindi ukiwaza kuwa haitakaa itokee mpendwa wetu akarudi tena. Hapo ndipo machozi humwagika kama mvua.

Kifo ni talaka ambayo tangu na tangu, haijazoeleka. Nafsi ya mtu inatupiga talaka tatu. Kifo! Si talaka rejea kwamba ipo siku atakuja mitaa ya Ukonga, Keko, Chang’ombe au sabasaba kutusabahi kiburudani. Imeenda sauti adhimu.

Mshituko wa watu kwa taarifa ya kifo chake ilikuwa ishara ya upendo wao kwake. Ni aina ya wanamuziki wenye sauti pekee yenye upekee. Mungu kaamua kuondoa kipaji hiki katika uso wa dunia hii. Apangalo halina makosa.

Aliishi na watu vizuri, ndo maana taarifa za kifo chake zilishitua wengi. Pengine kuliko ujio wa nyimbo zake mpya miaka kadhaa nyuma. Wasanii na Wabongo kwa ujumla, waliumia kusikia Maunda hatunaye.

Advertisement

Sauti, matamshi fasaha katika lugha zote mbili kiswahili na kiingereza. Vilifanya awe na upekee sana kisanii. Kifo chake pia wengi wetu kilitupa picha kamili, kwamba dada alikuwa na watu na alikuwa mtu wa watu.

Ili ujue hilo, alipata ajali akiwa njiani kurudi kwake akitokea kwenye msiba wa rafiki yake. Mashuhuda wengi wa saa chache kabla ya umauti wake, maelezo yao yanakupa picha hiyo, kuwa dada alikuwa mtu wa watu.

SOMA: Msanii Maunda Zorro afariki dunia

Lakini aina ya kifo chake, tunapata picha gani kwetu na wasanii wetu? Kifo ni kifo tu, na wakati wa Mungu ukifika hauna kinga. Lakini haituzuii kukitazama kifo cha Maunda kama somo kwetu na haswa wasanii.

James Dandu

Mwanamuziki James Dandu ‘Mtoto wa Dandu’, alifia maeneo ya Makumbusho baada kugongana uso kwa uso. Fred Marick ‘Mkoloni’ wa Wagosi wa Kaya, alikaririwa akisema ‘snika’ (raba). Ilifanya atambue kuwa ule ni mwili wa James Dandu.

Mchana wa jana yake alimuona na ile raba studio kwa Master Jay. Dandu alikuwa zaidi ya mwanamuziki, ndiye muanzilishi wa tuzo za muziki hapa Bongo. Ambazo kwa mara nyingine zimefanyika hivi karibuni. Yeye ndiye muasisi.

Taarifa zilizotolewa baadaye, zindai Dandu alitokea studip. Ambako yeye alikesha akitengeneza kazi zake. Hii ni kawaida kwa wanamuziki kufanya kazi usiku kwa sababu ya utulivu. Ni kwamba hutengeneza nyimbo usiku zaidi na kufanya shoo usiku zaidi.

Aiishi miaka mingi zaidi hukk nchini Sweden, akarudi Tanzania wakati muziki wa kizazi kipya ukianza kukimbiza. Ingawa aliishi kwa muda mfupi kabla ya kufariki, lakini yale mambo machache aliyoacha nyuma yamebaki kuwa alama kubwa katika muziki.


Complex na Vivie

Rapa na prodyuza Saimon Sayi ‘Complex’ na Vivian Tillya ‘Vivie’, ambaye alikuwa rapa na mtangazaji wa Clouds. Wote wawili wakiwa ni wachumba, tuliwapoteza kwa ajali ya gari. Walipata ajali wakitokea kwenye shoo za Fiesta.

Complex alikuwa mmoja wa wasanii wa mwanzoni kabisa. Ambao mbali ya kuchana mistari, walijikita katika kuunda midundo (bits). Yes! Alikuwa mkali kwenye eneo lote. Tulipoteza rapa mkali na prodyuza mkali.

Hata Vivian, kabla ya kushika maiki kama mtangazaji, alikuwa rapa wa kike. Alianza kuchana toka akiwa kwao Arusha na kuhamishia chimbo Dar. Poa ndiye aliyemshika B12 mkono na kumuachia kijiti pale XXL ya Clouds. Tulipoteza vipaji.

Sharo Milionea

Mkali wa hizi kazi toka kitaa cha Tanga, Sharo Milionea kifo chake ni ajali ya gari pia. Akiwa kwenye kilele cha juu zaidi cha umaarufu, Sharo alituacha Wabongo tukiwa bado na majonzi ya wasanii wengine kama Steven Kanumba.

Naye kaondoka akiwa bado kijana mdogo sana. Lakini mwenye kipaji cha kikubwa cha kuchekesha na hata muziki. Ni aina ya wasanii ambao ni ‘vesataili’ yaani ‘malti talentedi’. Ndo wale ambao wanaweza kufanya na kutenda lolote na popote.

Issa Kijoti

Kundi la taarabu la 5 Stars, likiwa na wakali kama Issa Kijoti. Umauti wao ulowakuta kwa ajali ya gari wakiwa vijana wadogo sana eneo la Mikumi, Morogoro. Wakiwa katika hatua za awali kabisa za kufaidi matunda ya sanaa wakatuacha.

Wakati huo Jahazi Modern Taarabu chini ya Mfalme Mzee Yusuf. Wakiwa hawagusiki kwa ubora na mtaji wa mashabiki wetu. Ndipo wakaibuka hawa vijana wa 5Stars, ambao kwa muda mfupi wakatikisa Ufalme wa Mzee Yusuf.

Mbaraka Mwishehe

Januari 2, 1979 mpiga gitaa, mtunzi, muimbaji, kiongozi na mmiliki wa bendi, Mbaraka Mwaluka Mwishehe, alifia hospitalini Mombasa, Kenya, baada ya kupata ajali ya gari. Huyu alikuwa ni zaidi ya staa kwa wakati ule. Mwamba kwelikweli alikuwa.

Ingawa mitazamo ya wengi hii leo, wanajenga picha kama alikuwa Mzee. Ukweli ni kwamba Mbaraka alikuwa na umri wa miaka 34 tu wakati anafariki. Alikuwa bado kijana mbichi kabisa na si mzee kama mtazamo wa wengi ulivyo.

Pamoja na umri mdogo, alikufa huku akiacha bendi kubwa ya muziki na wanamuziki. Mijengo Moro mjini na Dar. Akiburuzana kisanii na wakali wa wanamuziki barani Afrika, kama Franco Luambo Makiadi. Mbaraka alikuwa mtu na nusu.

Issa Matona

Issa Matona, gwiji la nyimbo za Pwani kutoka Zanzibar. Alifariki kwa ajali pia baada ya kugongwa na gari mitaa ya Upanga. Akitembea kuwahi shoo katika Ukumbi wa Diamond Jubilee. Huyu mwamba harusi zote za Bongo huimbwa nyimbo zake.

Matona alikuwa staa mkubwa sana Afrika Mashariki na kati na wale wanamuziki wa awali kuitangaza Zanzibar na Tanzania. Wakati Afrika ikiwa giza kuanzia Pemba Msumbiji hadi Malindi ya Kenya alikuwa staa mkubwa.

Kizazi hiki cha sasa ni vigumu sana kulifahamu jina la Gaby Katanga. Lakini wenye kuhusudu pigo zile za sebene wanalijua hili jina. Mmoja kati ya wapiga ‘dramzi’ bora sana kuwahi kuishi katika taifa hili. Alifariki baada ya ajali ya gari mitaa ya Kinondoni.

Kwa watu wa bendi, pale Manyanya (American Chips), ndiyo chimbo lao. Ni eneo ambalo chakula huuzwa mpaka asubuhi. Gaby na kina Mau Santiago walipata ajali wakiwa katika ‘pikapu’ wakielekea eneo hilo. Wakapinduka na Gaby kufariki.


Abou Semhando

Abou Semhando, kifo chake pia ni ajali ya pikipiki maeneo ya Mbezi. Akirejea nyumbani baada ya mishe zake za muziki. Alikuwa ni kiongozi wa Twanga Pepeta, kama ilivyo kwa Gaby Katanga naye alikuwa mpiga ‘dramzi’ mkongwe.

Abuu, alikuwa ni nguzo imara sana kwa Twanga Pepeta na kifo chake kilifanya hata uimara wa bendi hiyo kuanza kuteteleka kwa kasi. Alikuwa baba, mkongwe, kiongozi, mwalimu na msuluhishi kati ya wanamuziki na uongozi.

Kwa macho ya kawaida na si ya kiroho, kuna kitu cha kujifunza kwa wasanii wetu na hizi ajali. Kutokana na aina ya kazi yao. Kuna vitu lazima vipewe umakini sana kwa maisha ya wanamuziki wetu. Kazi ya muziki ina giza sana kuliko nuru.

Muda ambao watu wengi wamelala, wamepumzika na kuota ndoto. Wao ndo wapo mzigoni wakivuja jasho ili kuingiza kipato chao. Kazi zao za usiku usiku na kukeshakesha sana, ni pacha yaani kulwa na doto na ajali. Ndo ukweli wenyewe huo.

Hawa ni wasanii ambao waliondoka jumla jumla kwa ajali. Ajali ambazo asilimia 90 walipata wakiwa kazini. Wapo ambao walipata ajali wakiwa katika majukumu ya kazi yao, lakini dunia ikawapenda zaidi bado wapo hai.

Kuna Noorah ‘Baba Style’, alipata ajali usiku mnene akitokea maeneo ya kazi. Ajali ambayo ni chanzo kikuu cha kututenganisha Wabongo sisi na kipaji hiki kikubwa. Noorah ana dunia yake kwenye muziki wa kizazi kipya. Waulize wasanii wenzake.

Kuna Darassa ‘The Champion Boy’. Alipinduka na ndinga mara kadhaa huko kitaa cha kuelekea Shinyanga. Akiwahi shoo yake, baada ya muda kumtupa mkono na kila kona watu wakimuhitaji. Shoo kila baada ya shoo.

Twenty Parcent, naye kidogo apoteze uhai wake kwa ajali. Alilivaa lori moja lililokuwa limezimika njiani usiku bila uwepo wa alama yoyote. Ukiuliza alitokea wapi? Jibu ni Moro kwenye shoo akiwahi Dar kwenye shoo. Kazi juu ya kazi.

Kuna marehemu Tx Moshi William. Pia kabla ya umauti wake aliwahi kupata ajali mbaya sana ya gari. Hata wimbo akatunga kwa kumbukumbu ya ajali hiyo. Wote walikuwa kwenye majukumu ya kazi zao. Wapo ambao taarifa zao hazikuripotiwa au kusahaulika.

Kazi za muziki mara nyingi hufanyika nyakati za usiku. Kuanzia kuingia studio, shoo zenyewe pamoja na miadi na watu. Na muziki una urafiki zaidi na mitungi kwa wanamuziki wenyewe au mashabiki wao.

Kwa maana hiyo mwanamuziki akiwa mtungi ni hatari. Na akiwaburudisha watu wenye mitungi kichwani pia ni hatari. Mwanamuziki akiendesha gari akiwa mitungi ni hatari, na madereva wengi usiku wako mitungi. Ni hatari!

Anaweza kuwa si mnywaji, lakini ‘anadili’ na watu aina gani? Kuanzia pale kwenye shoo hadi barabarani, wakati wa kurudi majumbani? Hata kama mwanamuziki si mnywaji kama Muumini, vipi suala la uchovu?

Kuna haja ya kulitazama hili kwa upekee hasa kwa wasanii husika. Kutafuta madereva au kutenga muda wa kazi na muda wa kupumzisha mwili vyema. Ajali nyingi huchangia na uchovu ama haraka ya kuwahi kazi nyingine.

Advertisement