Msanii Maunda Zorro afariki dunia

Muktasari:

Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Maunda Zorro amefariki dunia baada ya kupata ajali ya gari jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Maunda Zorro amefariki dunia baada ya kupata ajali ya gari jijini Dar es Salaam.

Maunda aliyewahi kutikisa kwenye bongofleva kupitia nyimbo zake kadhaa ikiwemo ‘Nataka niwe wako’ na Mapenzi ni ya wawili’ amekumbwa na umauti usiku wa Jumatano Aprili 13, 2022.

Kwa mujibu wa Banana Zorro ambaye ni kaka wa marehemu, mdogo wake alifariki kufuatia ajali ya gari iliyotokea saa chache baada ya kuachana naye.
Banana ameeleza kuwa aliachana na Maunda saa 12 jioni baada ya kujumuika kwenye msiba wa rafiki yao wa muda mrefu.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa gari alilokuwa akiendesha Maunda liligongana na lori la mchanga na kusababisha umauti wake.
Saa nne usiku baada ya kuachana naye alipata taarifa za ajali na kifo cha mwanamuziki huyo kutoka kwenye familia ya mwanamuziki Zahir Ally Zorro.

"Familia ya Zahir Ally Zorro, tunasikitika kutangaza kifo cha binti/dada yetu Maunda Helleni Zorro kilichotokea jana kwa ajali ya gari Kigamboni Dar es Salaam.

"Taarifa zaidi tutatoa baadaye leo, msiba upo Maweni Kigamboni nyumbani kwa Mzee Zorro, Bwana alitoa  na Bwana ametwaa," amesema Banana kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Maunda ameacha watoto watatu.


Kwa taarifa zaidi endelea kufuatilia Mwananchi