Washauri matumizi ya teknolojia kukabili Uviko-19

Muktasari:

  • Wataalamu wa afya wamezishauri nchi za Afrika kuboresha mifumo ya utoaji huduma za afya na matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kukabiliana na majanga likiwemo la Uviko-19.

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wamezishauri nchi za Afrika kuboresha mifumo ya utoaji huduma za afya na matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kukabiliana na majanga kama la Uviko-19.

Wataalamu hayo jana Oktoba 12 katika mkutano ulioendeshwa kupitia mtandao wa Zoom uliojadili nafasi kwa jamii kutoa mawazo mapya yenye suluhisho la kudumu.

Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Afya ya Rocket Africa, Dk John Bwanika amesema, janga la Uviko-19 limetoa fursa na uhitaji wa nchi husika kuja na ubunifu katika sekta ya afya itakayoendana na mazingira yao.

Ametoa mfano wa teknolojia ya telemedicine akisema itasaidia wagonjwa kuwasiliana na daktari na kupata huduma bila kufika hospitali na hivyo kupunguza uwezekanao wa kupata maambukizi ya Uviko- 19.

“Fundisho kutokana na janga hili kwa nchi za Afrika, ni umuhimu wa kujikita katika matumizi ya afya mtandao (digital health) kupunguza misongamano ili kuepuka uwezekano wa kupata maambukizi mapya ikiwamo muda ambao mgonjwa anapoteza kusafiri hospitalini na kurudi nyumban,” amesema Dk Bwanika.

Ameongeza kuwa uzoefu umeonyesha kuwa kipindi cha wimbi la kwanza la ugonjwa huo, nchi za  Afrika zilikuwa na changamoto kubwa ya upungufu wa vifaa ikiwamo barakoa na madawa.


Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Utafiti kutoka Kituo cha Moyo cha Aswani (Aswan Heart Centre) cha nchini, Misri  Yasmine Aquib amesema ni wakati mwafaka kubuni na kufanya utafiti ili kukidhi mahitaji katika huduma afya.


Aquib alisema nchi za Afrika zinapaswa ziendeleze njia za kupima na upatikanaji wa vifaa vya kutosha vya kupima magonjwa. (Testing kits package)

“Janga la uviko-19 limebadilisha kabisa mfumo wa maisha ya watu. Ni wakati muafaka kwa wabunifu na watafiti kuja mbinu mbadala zitakasaid nchi hizi kutumia technoliojia kutoa huduma,” amesema.