Wasichana 3,000 waliokatisha masomo warejeshwa shuleni

Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Dk Michael Ng'umbi
Muktasari:
Jumla ya wasichana 3,333 (sawa asilimia 111) yenye umri wa kati ya miaka 13 hadi 21 waliokatisha masomo ya elimu ya sekondari kwa sababu mbalimbali wamerejeshwa shuleni mwaka 2021/2022.
Dodoma. Wasichana 3,333 (sawa asilimia 111) wenye umri kati ya miaka 13 hadi 21 waliokatisha masomo ya elimu ya sekondari kwa sababu mbalimbali wamerejeshwa shuleni mwaka 2021/2022.
Novemba 2021, aliyekuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alitangaza uamuzi wa Serikali wakuruhusu wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali kurejea shuleni.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima(TEWW), Dk Michael Ng’umbi ameyasema hayo wakati akielezea shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti ya 2022/2023.
Amesema wasichana hao ni wale waliokatisha masomo kutokana na mazingira magumu, kupata ujauzito au ndoa za utotoni.
“Tutajitahidi mwaka huu mwingine tujitahidi tupate namba hiyo hiyo ili waanze tena Januari mwakani,” amesema.
Dk Ng’umbi amesema programu hiyo ni kwa ajili ya wale waliokatiza masomo kwa wanafunzi wa sekondari tu.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali ambalo linajishughuliasha na Wanawake na Watoto (Wowap), Fatma Toufiq amesema hatua hiyo ni kubwa ya kuwawezesha wasichana hao kutimiza ndoto zao walizozikatisha kwasababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata ujauzito kutokana na kutokuwa na elimu sahihi ya afya ya uzazi.
“Tunamshukuru sana Rais Samia kwa kubali watoto hawa waweze kurejea shuleni. Hawa wamekuwa majasiri, hawakuogopa kunyanyapaliwa. Wanachotakiwa kufanya ni kufuata mambo yaliyowapeleka pale, wasirudie tena makosa kwasababu kutenda kosa si kosa bali kurudia kosa ndio kosa,”amesema Fatuma ambaye pia ni mbunge wa vitimaalum.