Wasimamizi miradi ya Uviko-19 watakiwa kuzingatia ubora

Muktasari:

  • Wasimamizi wa ujenzi  mradi wa kituo cha Afya cha mnyuzi Kilichopo katika Kata ya Mnyuzi wilayani Korogwe mkoani Tanga, wametakiwa kurekebisha haraka mapungufu yaliobainika kwenye ujenzi wa mradi huo.


Korogwe. Wasimamizi wa ujenzi  mradi wa kituo cha Afya cha mnyuzi Kilichopo katika Kata ya Mnyuzi wilayani Korogwe mkoani Tanga, wametakiwa kurekebisha haraka mapungufu yaliobainika kwenye ujenzi wa mradi huo.

Maekelezo hayo yametolewa na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2022 Sahili Geraruma wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika jengo hilo.

Mradi huo wa majengo ya kituo cha afya lenye thamani ya Sh 250 milioni limebainika kuwa na kasoro nyingi ambazo kwa mujibu wa Sahili zimetokana na uzembe wa wasimamiaji wa mradi wakati wa shughuli za ujenzi zikiendelea.

Amesema kasoro zilizobanika ni kukosekana kwa miundombinu ya kuchomea taka za hospitali, miundombinu ya kutiririshia maji wakati wa mvua na sehemu ya kunawia mikono.

"Mwenge wa Uhuru unatoa maelekezo kuwa miundombinu ya kuchomea taka ijengwe haraka kabla jengo halijaanza kutumika na kwa kuwa mmemaliza fedha zote mtajua pa kuzitoa nyingine lakini naagiza sehemu ya kuchomea taka iwepo kwa kuwa ilikuwepo kwenye bajeti ya Sh milioni 250,” amesema.

Licha ya mapungufu hayo, Sahili amesema kutokana na umuhimu wa kituo hicho kwa wananchi wa Mnyuzi Mwenge wa Uhuru uliridhia kuweka jiwe la msingi huku akisisitiza maagizo ya kufanyiwa kazi mapungufu yaliojitokeza.

Aidha amesema kumekuwa na changamoto ya kuchelewa kwa miradi  kunatokana na tabia ya uzembe inayofanywa na baadhi ya wakandarasi kutofuata taratibu za maombi ya kuongezewa muda.

"Mheshimiwa Rais ametoa fedha kwa ajili ya kuwajengea wananchi kituo cha afya ili kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo sasa ni wajibu kwa mnaopewa dhamana ya kusimamia miradi hii msimamie vizuri na  kwa uadilifu,” amesema.

Kwa upande wake kaimu Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kalist Lazaro amesema Mwenge wa Uhuru wilayani humo utazindua na kuweka mawe ya msingi pamoja na kukagua miradi saba yenye thamani ya Sh3.19 bilioni.