Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasimamizi, watekelezaji waja na mapendekezo kukamilisha miradi ya maendeleo

Wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Mbeya wakiwa katika warsha iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani humo kwa lengo kuwakumbusha kutimiza wajibu wao

Muktasari:

  • Warsha hiyo imeshirikisha wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo Mkoa wa Mbeya wakiwamo wakurugenzi, wakuu wa wilaya, wakuu wa idara ngazi za Wilaya na Mikoa iliyoandaliwa na Takukuru mkoani humo.

Mbeya. Wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo Mkoa wa Mbeya wamependekeza mambo kadhaa katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwamo tathimini na uwajibikaji.

Pia, wametaka uwapo wa ufuatiliaji na ushirikishwaji wa wananchi, misamaha ya kodi, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kuondoa shinikizo la kisiasa kwenye miradi katika baadhi ya maeneo na bajeti husika kutumika kwenye sehemu elekezi.

Hayo yamebainishwa leo Julai 9,2026 katika warsha ya wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani humo.

Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Mbeya, Ndege Filbert amesema ili baadhi ya miradi ikiwamo barabara inakuwa chini ya kiwango licha ya ufuatiliaji, uchambuzi na utambuzi unaofanywa katika maeneo ya miradi.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa akizungumza leo Julai 9, 2026 katika warsha ya wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani humo.

“Lakini unakuta baadhi ya miradi mfano barabara ni ya hovyo, nishauri Takukuru muongeze kipengele cha tathimini na uwajibikaji ili akikutwa mtu ametupitisha kwenye eneo lake akabainika awajibishwe,” amesema Filbert.

Kwa upande wake Meneja Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Paschal Manono amesema tathimini na ufuatiliaji isaidie kujipanga na mwaka wa fedha, akieleza kuwa ipo baadhi ya miradi inayokwama kutekelezeka.

“Tunapotengeneza bajeti tuzingatie ile miradi inayokuwa imesimama, tunapoweka bajeti na miradi mingine tunachelewesha ile ya awali, kupanga ni kitu kimoja na utekelezaji ni kitu kingine, tujikite kwenye ukamilishaji wa miradi ya awali,” amesema Manono.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mbeya, Simon Bukuku ameshauri Takukuru kuwafikia watendaji ofisini kwao kujadiliana masuala utekelezaji wa miradi na kushauriana changamoto kabla ya kusubiri kutokea tatizo.

Naye Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Kyela, Venance Sangawe amesema baadhi ya miradi inalazimishwa kisiasa akieleza kuwa wataalamu lazima waiweke kwenye maandishi ili wanaolazimisha kisiasa wasifanikiwe.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mbeya, Maghela Ndimbo akizungumza leo Julai 9, 2026 katika warsha ya wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani humo.

“Miradi mingi inachelewa hata kabla haijaanza, mazingira na bei husika inakuwa tofauti, kwa hali hiyo lazima mradi uchelewe wahandisi kila Wilaya lazima wafanye wenyewe” amesema Sangawe.

Awali, akifungua warsha hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa ameishukuru Takukuru kwa kuandaa kikao hicho akieleza kuwa kisiwe mwisho badala yake iwe endelevu katika kujengeana uwezo wataalamu.

“Lazima tujadili kwa pamoja mambo haya muhimu, tujue upana wa dhana ya rushwa, kuna haja ya kutoa elimu kuhusu rushwa, wananchi wanajua kinachofanyika huko kwenye jamii hivyo hizi warsha zisiishie leo bali ziwe endelevu tukumbushane” amesema Malisa.

Kwa upande wake Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mbeya, Maghela Ndimbo amesema lengo la warsha hiyo ni kuwakumbusha watendaji na wasimamizi wa miradi kuzingatia mwongozo wa utekelezaji wa majukumu yao.

“Lazima kuwepo ushirikishwaji wa wananchi katika utekelezaji wa miradi, fedha inayotolewa iendane na thamani ya mradi husika, kusiwepo na ucheleweshaji wa miradi pale fedha inapokuwapo na fedha zielekezwe eneo husika,” amesema Ndimbo.