Wasiwasi watanda kampuni ya Qnet

Wasiwasi watanda kampuni ya Qnet

Muktasari:

Kila kona sasa ni kilio cha wananchi kutapeliwa mamilioni ya fedha. Wapo waliofikia hatua hata ya kuacha kazi, hasa watumishi wa umma kwa ahadi tamutamu za kuvuna fedha kutoka kampuni ya biashara za mtandao ya Qnet.

Dar es Salaam. Kila kona sasa ni kilio cha wananchi kutapeliwa mamilioni ya fedha. Wapo waliofikia hatua hata ya kuacha kazi, hasa watumishi wa umma kwa ahadi tamutamu za kuvuna fedha kutoka kampuni ya biashara za mtandao ya Qnet.

Baada ya kukithiri kwa madai ya wananchi na kuongezeka kwa mijadala kwenye mitandao ya kijamii, kufuatia gazeti hili kuweka wazi kilio cha wananchi wakidai kutapeliwa na kampuni hiyo mkoani Kilimanjaro, Jeshi la Polisi limeamua kuingilia kati.

Akizungumza jana na Mwananchi kwa simu, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi, Robert Boaz alisema jeshi hilo limeanzisha uchunguzi kwa kampuni ya QNet baada ya kupokea malalamiko mengi ya watu kutapeliwa na kampuni hiyo.


“Tumeshapokea malalamiko mengi, kuna uchunguzi tunaufanya kuhusu QNet jinsi wanavyofanya shughuli zao,” alisema Boaz huku akitahadharisha wananchi kuepuka biashara za upatu.

“Basically (kimsingi), Pyramid scheme (upatu) ni kosa la jinai, kwa sababu mnapoanza mnakuwa wachache na mnaweza mkalipana kidogo kwa kuchangiana. Kama mko wawili watatu na kama sharti mlipwe na waliochini, maana yake mtalipana na mkatoana.

“Lakini kadiri idadi inavyokuwa kubwa ndivyo inavyokuwa vigumu kulipana, kwa hiyo kuna watu ambao hatalipwa. Kwa msingi huo kitendo hicho kiliharamishwa kwa mujibu wa sheria” alisema Kamishna Boaz.

Aliwatahadharisha wananchi kuepuka michezo ya upatu inayowatamanisha kupata fedha za haraka.

“Kwa hiyo QNet kuna uchunguzi mpana kuhusu suala hilo na niwa encourage (niwatie moyo) wananchi wanaodhani kuwa wamehujumiwa waripoti hasa kwenye mikoa ambayo kuna wataalamu wa kuangalia masuala hayo,” alisema.

Maelezo yanaonyesha Qnet ni kampuni ya kimataifa inayofanya biashara za masoko ya mitandaoni kwa kuunganisha wateja na kuwauzia bidhaa.

Waeleza walivyolizwa

Miongoni mwa watu walioilalamikia QNet ni Janet Julius mkazi wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro aliyedai kutapeliwa Sh4.3 milioni alizodai kumpa ofisa ugani huyo.

Maelezo ya Janet aliyekuwa akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya yalisababisha mkuu huyo kuagizwa kukamatwa kwa ofisa ugavi wa Manispaa ya Moshi, Diminic Mwapombe kwa kuhusishwa na ukusanyaji wa fedha kutoka kwa wateja wa QNet.

“Alikuja rafiki yangu ananiambia kuna wafanyabiashara wa QNet ambapo kiwango cha chini cha kuwekeza ni Sh4.3 milioni, ambapo ukitoa unapewa cheni na saa ya mkononi.

“Baada ya hapo nitakuwa naingiziwa dola 200 kwenye akaunti yangu. Nikawaambia sawa, nikakopa fedha nikawapa taslimu. Tangu hapo hakuna kinachoendelea, nimewaomba wanipe hata risiti wanasema ziko kwenye mtandao na zinatoka Malaysia. Wamenionyesha picha nyingi walizopiga na viongozi wa Serikali.

Kwa mujibu wa Sabaya, QNet imechukua fedha za watumishi wengi wilayani humo wakiwamo walimu kwa madai ya kuwaingizia faida kwenye akaunti zao.

Mtu mwingine aliyezungumza na Mwananchi jana jijini Dar es Salaam kwa sharti la kutotajwa jina lake, alisema aliifahamu kampuni hiyo tangu mwaka 2017 na alishawishiwa kujiunga nayo, lakini baadaye alishtuka akaacha.

“Nilikuwa na rafiki yangu ambaye ni Mbunge (anamtaja) alinishawishi kujiunga, akaniambia niende kwenye ofisi za QNet zilizopo Oysterbay ili nikapewe maelezo,” alisema.

Aliendelea kusema kuwa baada ya kufika alikutana na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Khan ambaye alimshawishi kujiunga huku akimuonyesha bidhaa wanazouza ikiwa pamoja na saa.

“Niliposikiliza maelezo ya Khan nikamwomba muda nifikirie, kwa sababu hata hela yenyewe sikuwa nayo,’ alisema.

Alisema baadaye alishawishiwa na rafiki zake kuhusu biashara hiyo, hadi alipokutana na rafiki mwingine aliyemshauri aachane nayo.

Khan alipotafutwa kwa simu alikiri kuifahamu QNet, lakini akasema kwa sasa ameshaachana nayo.

“Niliachana nao miaka mingi sana,” alisema Khan huku akitaka kujua nani aliyetoa taarifa zake.

Mtu mwingine ambaye pia aliomba asitajwe jina gazetini, alisema alishawishiwa na wafuasi wa QNet na kutoa fedha kiasi cha Sh4.3 milioni, lakini hakupata faida.

“Nimekuja kugundua kuwa ile ni biashara haramu tu. Kwa sababu ukishatoa fedha kama Sh4.3 milioni au Sh6 milioni au hata Sh10 milioni wanakupa saa au suti au wanakupa ofa ya kwenda kustarehe kwenye hoteli wanazofanya nazo kazi ambako hulipa nusu ya gharama.

Mwananchi ilifanya juhudi za kuwapata wawakilishi wa kampuni hiyo kwa kutafuta ofisi yao. Miongoni mwa watu waliotajwa kuhamasisha wateja wa kampuni hiyo ni Nancy Assenga na alipotafutwa kwa simu alimtaka mwandishi kwenda ofisini kwa ajili ya taarifa zaidi.

Mwandishi alifika katika ofisi hiyo iliyopo ghorofa la 15 katika jengo la Bandari jijini Dar es Salaam, hata hivyo hapakuwepo na ofisi yenye jina la QNet, badala yake kulikuwa na ofisi ya kampuni ya Sted International.

Mhudumu wa ofisi hiyo ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema QNet ni miongoni mwa wateja wao wanaowaingizia mizigo yao kutoka Malaysia.

“Hapa tunahifadhi mizigo ya QNet, lakini wenyewe hawapo, si unajua hiyo ni Network marketing (biashara ya mtandao)?” alieleza.

“Kama una malalamiko kuhusu QNet wana mwanasheria wao,” alisema mhudumu huyo huku pia akikataa kutoa mawasiliano ya mwanasheria huyo.