Wasomi wahimizwa kuleta maendeleo chanya katika jamii
Muktasari:
- Wito huo umetolewa leo Novemba 30, 2024 jijini Dar es Salaam na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye katika mahafali ya 54 ya chuo hicho.
Dar es Salaam. Wahitimu wa vyuo vikuu nchini wamehimizwa kutumia taaluma waliyoipata, kutoa ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ndani na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa leo Novemba 30, 2024 jijini Dar es Salaam na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye katika mahafali ya 54 ya chuo hicho.
Anangisye amewasisitiza kuwa wepesi kuangalia sehemu nyingine ambapo maarifa na ujuzi wao unaweza kutumika kwa ufanisi zaidi kuliko kusubiri ajira serikalini au katika sekta binafsi.
"Muwe watu wa kutafuta fursa badala ya kusubiri fursa ziwafuate, jambo ambalo si rahisi kutokea katika dunia ya leo ambayo ni kijiji chenye ushindani mkubwa.
Aidha, amewakumbusha wahitimu kuwa wazalendo kwa nchi, kudumisha tunu za amani, umoja, mshikamano wa nchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa chuo hicho, Rais mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete amesema anafurahishwa kuona ongezeko la idadi ya wahitimu katika ngazi za uzamivu, huku akiwahimiza kutumia elimu yao katika kuleta mapinduzi kwenye sekta mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Katika mahafali hayo ya 54, jumla ya wahitimu 55 walitunukiwa shahada ya uzamivu kati yao 38 ni wanaume na 17 ni wanawake ambao ni sawa na asilimia 31.
Naye Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho Balozi Mwanaidi Maajar, amewasisitizia kwenda kudhihirisha taaluma zao kwa vitendo kwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.
Amesema baraza linaendelea kuwasisitiza wazazi na walezi kusimamia misingi bora ya malezi kwa watoto hasa katika kipindi hiki cha utandawazi, kwani bila kufanya hivyo kutakuwa na kizazi tegemezi ambacho hakiwezi kuwajibika ipasavyo.
"Ninaisihi jamii na taasisi mbalimbali zikiwemo za kidini, kurudi kwenye misingi bora ya malezi kwa kuliangalia suala hili kwa jicho la kipekee ili kulinusuru taifa letu la kesho na madhara yatokanayo na kizazi kisichowajibika," amesema Balozi Maajar.