Wataalamu: Ujauzito usimzuie mama kunyonyesha

MAMA NA MWANA: Uchunguzi unaonyesha asilimia 86 ya vifo vya watoto vinasababishwa na wanawake wanaokwepa kulea ujauzito au kunyonyesha kwa kuamini maziwa yamechafuka. PICHA | AFP

Muktasari:

  • Uchunguzi mwingine unaonyesha kwamba asilimia 86 ya vifo vya watoto, vikiwamo vya utoaji mimba, vinasababishwa na wanawake wanaokwepa kulea ujauzito au kuendelea kunyonyesha kwa fikra potofu kuwa maziwa yamechafuka.

Dar es Salaam. Uchunguzi wa kitaalamu unaonyesha kwamba hakuna madhara kwa mwanamke kuendelea kumnyonyesha mtoto mchanga iwapo atajikuta amepata ujauzito.

Hayo yamebainika wakati uchunguzi mwingine unaonyesha kwamba asilimia 86 ya vifo vya watoto, vikiwamo vya utoaji mimba, vinasababishwa na wanawake wanaokwepa kulea ujauzito au kuendelea kunyonyesha kwa fikra potofu kuwa maziwa yamechafuka.

Hayo yamesemwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (Mewata), Dk Caroline Mayengo kwenye mahojiano na gazeti hili.

“Hakuna madhara yoyote kwa mama mjamzito kuendelea kunyonyesha. Mtoto aliyeko tumboni na mtoto mwingine ambaye bado ananyonya wataendelea kukua vizuri,” alisema.

Alifafanua kuwa, iwapo mwanamke yeyote atabaini amepata ujauzito wakati akiwa bado ana mtoto mchanga ataendelea kumnyonyesha hadi mimba itakapofikia umri wa miezi saba.

Ila ameonya kuwa mwanamke anayenyonyesha huku akiwa ni mjamzito anapaswa kutunzwa vizuri zaidi kwa kupatiwa vyakula bora vya kutosha ili kujitunza binafsi na watoto anaowalea.

“Mtoto asiachishwe kunyonyeshwa kwa sababu mama ni mjamzito… Hali ya utapiamlo ya mama ndiyo inaweza kumwathiri mtoto lakini kama anapata chakula cha kutosha hakuna madhara,” alisema Dk Mayengo.

Kuhusu vyakula, alisema mama mjamzito anapaswa kula vyakula vyote muhimu vikiwamo vya vitamini, madini na vya protini kwa ajili ya kujenga mwili na madini mbalimbali mwilini.

Alisema kitaalamu inashauriwa mtoto mmoja anapozaliwa hadi kupata mimba ya mtoto wa pili angalau wapishane kwa miaka miwili.

“Kama mama akibeba mimba nyingine chini ya miaka miaka miwili(care)utunzaji  wa mtoto mwingine unakuwa si kubwa sana na ukiangalia watoto wanaokufa utakuta mama zao wana watoto wengine wachanga,”alisema.

Alisema kumekuwa na kupishana kwa watoto ambako hakuendani na taratibu za kiafya hivyo alishauri watu kutumia huduma za uzazi wa mpango ili kutoa nafasi kati ya mtoto mmoja hadi mwingine.

Hata hivyo alisema baadhi ya watu wamekuwa wakieneza mitazamo hasi juu ya uzazi wa mpango wakati ukweli ni kwamba manufaa ni mengi.

Alisema kwa wastani nchini wanawake 8,000 wanakufa kila mwaka kutokana na matatizo ya uzazi ukichangiwa pia na  ongezeko  la utoaji mimba haramu.

Katibu wa Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania (PAT), Dk Namala Mkopi alionya  wanawake waepuke kubeba mimba bila kuwa na utaratibu mzuri unaoruhusu malezi bora.

“Kama hatutaweza kusimama vizuri kwenye uzazi wa mpango tutakuwa tunawatesa watoto na kinamama kwa sababu wao ndiyo wahangaikaji wakubwa kwenye familia,”alisema Dk Mkopi.

Baadhi ya watu mitaani wamekuwa wakizungumzia kuhusu suala la maziwa kuchafuka wakati wanawake wanapobeba mimba huku wakidai kuwa hali hiyo inasababisha watoto kubemendwa.

Dk Mkopi alielezea hali hiyo akisema mimba haina uhusiano wowote na kumharibu mtoto anayenyonya.