Wataka Kiswahili kitumike mahakamani

Muktasari:

Serikali imetakiwa kuweka utaratibu wa matumizi ya lugha ya Kiswahili ili itumike hasa kwenye utoaji wa haki ikiwemo mhimili wa Mahakama, badala ya matumzi ya Kiingereza ambacho hakieleweki kwa wananchi walio wengi.

Bukombe. Serikali imetakiwa kuweka utaratibu wa matumizi ya lugha ya Kiswahili ili itumike hasa kwenye utoaji wa haki ikiwemo mhimili wa Mahakama, badala ya matumzi ya Kiingereza ambacho hakieleweki kwa wananchi walio wengi.

Ombi hilo limetolewa leo Desemba 9, 2022 na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Wilaya ya Bukombe, Hames Ngalama wakati akichagia maoni kwenye mjadala wa maadhimisho ya sherehe ya miaka 61 ya uhuru uliofanyika kimkoa wilayani hapa.

"Watanzania walitumikishwa na Waingereza wakati wanatutawala baadaye tuliwaondoa na bado tunatumia lugha yao kwenye mhimili wa kutafasiri sheria ambao ni Mahakama, tena mbaya zaidi hukumu mahakamani kwa wananchi zinatatolewa kwa lugha ya Kingereza badala ya Kiswahili," amesema Ngalama.

Ngalama ameiomba Serikali kulionea umuhimu jambo hilo ili wakati wa Tanzania wanasherekea miaka 61 ya Uhuru wa nchi yao, wafurahie kuona Kiswahili kikitumika Mahakamani.

Tayari Mahakama imeshatangaza kuanza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mienendo ya kesi.

Mbali na lugha, baadhi ya wazee waliokuwepo kwwnye mdahalo huo walitoa kilio cha kukosa huduma za afya.

Eliezer Mishai (82) amesema licha ya Serikali kutangaza kutoa huduma za afya bure kwa wazee kuwa na madirisha yao hospitalini, agizo hilo halitekelezwi.

"Serikali ilianzisha madirisha ya dawa za wazee leo hii hayo madirisha hayapo na wazee wanahangaika, kupata matibabu,” amesema.


Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Lutengano Mwalwiba amesema dirisha la dawa za wazee kwa hospitali ya wilaya hiyo lipo, ila kuna changamoto uhaba wa dawa kutokana na ufinyu wa bajeti ya dawa.