Watakiwa kujitolea kusaidia waathirika wa mafuriko

Mkuu wa Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Meja Edward Gowele (kushoto) akisalimiana na mwakilishi wa Lions Club International Tanzania, Muntazir Barwan, baada ya kupokea misaada kwa ajili ya waathirika wa mafuriko. Picha na Ammar Masimba.

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Major Edward Gowele amesema tangu mafuriko yalipotokea, kuna zaidi ya watu 89,000 walioathirika kwa kukosa makazi, huku nyumba 628 zikibomoka.

Dar es Salaam. Wakati bado athari za mafuriko wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani zikiendelea kuathiri maelfu ya wananchi, Watanzania wametakiwa kujitolea kuwasadia kwa hali na mali wanaanchi hao.

Wito huo umetolewa Mei 4, 2024 na wawakilishi wa taasisi za Lions Club na Who is Hussein walipokuwa wakitoa misaada kwa waathirika wa mafuriko wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani.

Akizunguza baada ya kutoa misaada hiyo, Gavana wa Lions Club International Tanzania, Happiness Nkya, amesema klabu hiyo imeguswa na hali mbaya za kibinadamu zilizowapata waathirika wa mafuriko.

“Kwanza tulihamasisha wenzetu kuchanga na pia tuliandika barua makao makuu Marekani tukiomba msada wa dharura.

“Wito wetu kwa Watanzania ni kujitoa kwa wenzetu wa Rufiji walioathirika. Tumesikia pia wenzetu wa Morogoro nao wameathirina na mafuriko na maeneo mengine nchini, hivyo tunatoa wito watu wajitokeze wajitokeze kuchangia,” amesema.

Amesema klabu hiyo ina wanachama zaidi ya 600 katika klabu 23 zilizopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Morogoro.

Misaada waliyotoa ni pamoja na sukari kilo 1,000, sembe kilo 1,000, maharage kilo 1,000, mchele kilo 1,000 mafuta ya kupikia lita 600, mablangeti 800, foronya 400 mikeka 210 na mbegu za mahindi kilo 400.


Kwa upande wake,  Mohsin Barwan wa taasisi ya Who is Hussein amesema wameguswa na adha inayowapata wananchi wa Rufiji, ndio maana wamejitokeza kuchangia.

“Sisi tumeguswa na hili jambo baada kuona Mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa ametoa fedha zake za mfukoni, wakati alipaswa achukue ile kero na kuwapelekea wafadhili.

“Ndipo tukaanza kuchangishana ili kumuunga mbunge na Rais (Samia Suluhu Hassan) aliyetoa chakula karibu tani 300.”

Amesema wametoa misada yenye thamani ya Sh28 milioni ambayo ni pamoja na mchele kilo 2,000, sembe kilo 1,500, sukari kilo 1,400 mafuta lita 1,200, maharage kilo 900, sabuni, dawa za meno, miswaki, magodoro 110, maji na taulo za kike.

Akipokea misaada hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele amesema mpaka sasa kuna zaidi ya watu 89,000 walioathirika na mafuriko na nyumba 628 zilizoathiriwa na mafuriko hayo.

“Wapo watu waliokuwa wamezingizwa na maji, hivyo, vyombo vya ulinzi na usalama vilifika hayo maeneo, kulikuwa na Jeshi la Wananchi (JWTZ) na Jeshi la Zimamoto walikwenda kuwatoa kwenye maeneo hatarishi.

“Vinginevyo, leo tusingekuwa tunazungumzia kuleta chakula, tungekuwa tunazungumzia makaburi tuliyonayo,” amesema.

Mbali na kuwashukuru wafadhili kwa misada yao, amesema bado wanahitaji misaada ya kijamii na kibinadamu ni wengi.

Akieleza mipango ya muda mrefu, DC Gowele amesema Serikali imetoa eneo lililokuwa msitu wa hifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na kukata viwanja zaidi ya 600 ili kuwahamisha wananchi walio kwenye maeneo hatarishi.