Watakiwa kula zaidi vyakula vya asili kujikinga na magonjwa

Muktasari:

  • Katika kampeni hiyo ya upimaji inayoitwa ‘Dk Samia Suluhu Hassan Tiba Mkoba’, inayotekelezwa na Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jumla ya watu 307 wamepimwa magonjwa ya moyo na miongoni mwao, 37 wamepelekwa kwenye matibabu zaidi.

Siha. Wananchi mkoani Kilimanjaro wametakiwa kutumia zaidi vyakula vya asili ili kujilinda na magonjwa yasiyoambukiza kikiwamo kisukari na shinikizo la damu, kwani matibabu yake ni gharama kubwa.

Wito huo umetolewa leo Desemba 22 katika Hospitali ya Wilaya ya Siha  katika kampeni ya upimaji wa afya inayoitwa ‘Dk Samia Suluhu Hassan Tiba Mkoba’, inayotekelezwa na Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ambapo watu 307 wamepimwa.

Wakizungumza wakati upimaji huo ukiendelea, baadhi ya wananchi akiwamo Muhamed Mzava mkazi wa Sanya Juu, ameiomba Serikali kuweka mkakati utakaowezesha kutumia vyakula vya asili.

"Mmesikia kwamba gharama za kumwona daktari bingwa ni Sh2.7 milioni, lakini kwa nini tufike huko,  tule vyakula hivyo ikiwamo matunda na mboga za majani, kuzuia ni bora kuliko tiba," amesama Mzava.

Akizungumza katika shughuli hiyo, Naibu Waziri wa Afya, Godwin Mollel amewataka watumishi wa afya katika hospitali hiyo kutoa huduma bora na lugha nzuri kwa wagonjwa.

Dk Mollel pia amekabidhi gari moja kwa Mganga Mkuu wa wilaya na vifaa tiba hospitalini hapo.

Akipokea msaada huo, Mkurungenzi Mtendaji wa halmshauri hiyo, Dk Haji Mnasi ameishukuru Serikali hasa kwa kutoa matibabu ya awali ya moyo bure kwa wananchi, pia kuleta vifaa tiba, gari moja kwa ajili ya mganga mkuu wa wilaya na ahadi ya kupeleka magari mawili ya wagonjwa.

Naye daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI, Belila Kimambo amesema kuanzia Desemba 18 hadi 21 mwaka huu, jumla ya wagonjwa 307 wamepimwa na 37 wamepewa rufaa ya kwenda kupata matibabu zaidi kwenye taasisi hiyo iliyopo jijini Dar esalaam.