Watalii Ibanda-Kyerwa walia na ubovu miundombinu

Baadhi ya watalii wakisukuma gari baada ya kukwama hifadhini wakati wakifanya utalii hifadhi ya Ibanda-Kyerwa. Picha na Alodia Dominick.

Muktasari:

Baadhi ya watalii waliotembelea hifadhi ya Taifa ya Ibanda-Kyerwa mkoani Kagera wameomba Serikali kutatua changamoto zilizopo kwenye hifadhi hiyo ikiwa ni pamoja na kutengeneza miundombinu ya barabara na kuweka wanyama katika hifadhi hiyo kutoka hifadhi nyingine.

Kyerwa. Baadhi ya watalii waliotembelea hifadhi ya Taifa ya Ibanda-Kyerwa mkoani Kagera wameomba Serikali kutatua changamoto zilizopo kwenye hifadhi hiyo ikiwa ni pamoja na kutengeneza miundombinu ya barabara na kuweka wanyama katika hifadhi hiyo kutoka hifadhi nyingine.

Rai hiyo imetolewa Mei 14, 2022 wakati watalii hao wakiwa kwenye uzinduzi wa kampeni ya mama yangu nchi yangu ya kuhamasisha utalii iliofanyika katika hifadhi ya Ibanda-Kyerwa baada ya magari waliyokuwa wamepanda kukwama hifadhini kutokana na barabara kutomwagwa changarawe.

Mtalii kutoka Wilaya ya Biharamlo, Anthony Paul amesema Serikali inapaswa kumwaga changarawe kwenye barabara ili watalii wanapoingia kwenye hifadhi wasikwame.

"Leo nimetembelea hifadhi hii ya Ibanda-Kyerwa lakini pamoja na watalii wengine tumeshuhudia magari yakikwama kutokana na barabara kutomwagwa changalawe hivyo nishauri mamlaka husika kutengeneza miundombinu ya barabara katika hifadhi hii" amesema Paul

Mtalii kutoka Bukoba mjini, Neema Safari amesema ili hifadhi hiyo iweze kupata watalii, Tanapa inapaswa kuhamisha wanyama kutoka hifadhi nyingine na kuwahamishia humo ili watalii wanapotembelea hifadhi hiyo waone wanyama mbalimbali.

Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Rashid Mwaimu ameahidi kuwa Serikali kwa kushirikiana na Tanapa watatafuta ufumbuzi wa miundombinu ya barabara.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi (ACC) katika hifadhi za Taifa za Ibanda-Kyerwa na Rumanyika-Karagwe, Moronda B Moronda akizungumza na watalii amesema kuwa, hifadhi ya Ibanda-Kyerwa wanapatikana wanyama aina ya Korongo ambao ni jamii ya swala.

Amesema anahamaisha wananchi wa Kagera na maeneo ya jirani  kuja kutembelea hifadhi za mkoa huo ambazo ni tatu, Ibanda-Kyerwa, Rumanyika-Karagwe na Burigi-Chato.