Watano mbaroni Katavi wakituhumiwa wizi wa vifaa vya kieletroniki

Kamanda wa polisi mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani akionesha baadhi ya vitu vilivyokamatwa. Picha na Mary Clemence
Katavi. Jeshi la polisi mkoani Katavi linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kuiba televisheni 10, redio tatu na kompyuta moja.
Akizungumza na wanahabari leo Julai 2, 2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani amesema watuhumiwa hao wamepatikana baada ya wananchi kutoa taarifa kwa jeshi la polisi.
"Wananchi walitoa taarifa za siri tunawashukru sana, polisi walifanya misako kweli wakawakamata watuhumiwa hao wakiwa na mali za wizi," amesema.
Amewajata watuhumiwa hao kuwa ni Daud Talinga (50), Erick Richard (28), Emmanuel John (37), Joel Lameck (50) na Telena Richard (28) wote wakazi wa Manispaa ya Mpanda.
“Watuhumiwa wote wapo Kituo cha Polisi mjini Mpanda, tunaendelea na uchunguzi kubaini kama wanashiriki pia vitendo vingine vya kihalifu, upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani,”amesema Ngonyani.
Aidha amewaomba wananchi walioibiwa televisheni, redio na vingine kujitokeza wakiwa na vielelezo ili kuchukua mali zao huku akiwataka kuendelea kutoa ushirikiano kuwafichua wahalifu.