Watano wafa ajalini, mmoja ajeruhiwa

Muktasari:

  • Watu watano wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea leo Jumatano Septemba 08, 2021 saa 10 alfajiri katika barabara ya Arusha na Moshi eneo la Konoike Kijiji cha Kolila wilayani  Arumeru .

Arusha. Watu watano wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea leo Jumatano Septemba 08, 2021 saa 10 alfajiri katika barabara ya Arusha na Moshi eneo la Konoike Kijiji cha Kolila wilayani  Arumeru .

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso wakati gari lenye namba za usajili T.111 CUU aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa linaendeshwa na Heriel Jinja Lyimo(42)mkazi wa Holili mkoani Kilimanjaro kugongana na gari lenye namba za usajili T.612 BNN aina ya Mitsubishi Canter iliyokuwa ikiendeshwa na Peter Mmasi.

Masejo  amesema uchunguzi wa awali umebaini kwamba chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari aina ya Mitsubishi Fuso iliyokuwa inatokea Moshi kuelekea Arusha na inadaiwa  dereva alihamia upande wa pili wa barabara na kugongana na Mitsubishi Canter.


“Baada ya ajali hiyo kutokea  gari aina Mitsubishi Fuso lilipitiliza na kuanguka kwenye mtaro uliopo pembezoni mwa barabara hiyo,”amesema Masejo

 Amewataja waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni Peter Mmasi ambaye ni dereva wa gari aina ya Mitsubishi Canter,Victor Kileo,Vivian Urio na Isack Temba ambao walikuwa abiria kwenye  gari hilo ambao ni wakazi wa Baraa jijini Arusha.

 Pia kwenye  gari aina ya Mitsubish Fuso aliyefariki ni utingo wa gari hiyo aliyefahamika kwa jina moja la Idd mkazi wa Himo mkoani Kilimanjaro.

 Kamanda Masejo amesema majeruhi katika ajali hiyo ni Heriel Jinja Lyimo amepelekwa katika hospitali ya rufaa KCMC mkoani Kilimanjaro kwaajili ya matibabu zaidi na miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Mount Meru jijini Arusha.

Kamanda huyo ametoa wito kwa madereva na watumiaji wa barabara kuwa makini na matumizi sahihi ya alama za usalama barabarani ili kuepusha madhara makubwa kwa binadamu na mali zao .