Watanzania watakiwa kula vyakula vya asili


Muktasari:

Tamasha la vyakula asilia lanafanyika Mbagala jijini Dar es Salaam ambapo watu wajitokeza kupika vyakula vye asili vya makabila mbalimbali.

Dar es Salaam. Wakati suala la udumavu na ukosefu wa lishe likiendelea kushika kasi nchini, Watanzania wametakiwa kuachana na vyakula vya kusindikwa na vyenye mafuta mengi na badala yake wageukie vyakula vya asili ambavyo kwa kiasi kikubwa vina virutubisho muhimu kwa mwili wa binadamu.

Hayo yameelezwa na mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), Charles Tulai wakati wa tamasha la vyakula vya asili linaofahamika kama Msosi Asilia lililofanyika leo Jumapili Oktoba 23, 2022 Mbagala jijini Dar es Salaam.

Tulai ameeleza kuwa katika miaka ya karibuni hali ya lishe katika mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania haiko vizuri kutokana watu kula vyakula visivyokuwa na virutubisho.

Amesema kutokana na hilo FAO kupitia mradi wake wa Afri Connect imeona kuna haja ya kuweka mkazo kwenye suala la lishe na ndiyo sababu ikawezesha kufanyika kwa tamasha hilo la kuhamasisha vyakula vya asili.

“Tunaposema kuimarisha afya bora ya binadamu lishe inahusika na hapa ndipo tunapokuja kwenye vyakula vyetu vya asili ambavyo kwa uhalisia ndivyo vyenye virutubisho. Hebu turudi katika vyakula hivi ambavyo wengi vimetukuza lakini kutokana na maendeleo ya teknolojia tukaviacha na kugeukia vitu vya kusindikwa,”

Kwa upande wake mwanzilishi wa taasisi ya Agri Thamani, Neema Lugangira amesema tamasha hilo limefanyika kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa vyakula vya asili ambavyo kwa kiasi kikubwa vimepoteza thamani yake.

“Kuna baadhi ya vyakula vimeachwa kabisa, yani mtoto tangu amezaliwa anakula vyakula vya kufungasha, sawa inaweza kuonekana ni vizuri lakini vipi kuhusu umuhimu wake kwenye afya. Tunapozungumzia vyakula vya asili hivi vina virutubisho muhimu kuanzia kwenye ukuaji hadi ujengaji wa ubongo,”.

Mama lishe na baba lishe walijitokeza kwa wingi kwenye tamasha hilo wakipika vyakula vya asili ya makabila mbalimbali kwa mitindo ya upishi wa asili usiohusisha viungo na mafuta.