Watanzania watakiwa kutoa ushirikiano mapambano ya rushwa

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Sahili Geraruma akizungumza na wananchi wa kata ya Msente wilayani Kilindi kuhusu umuhimu wa wakushiriki katika mapambano dhidi Rushwa. Picha na Susan Uhinga

Muktasari:

Watanzania wametakiwa kutoa ushirikilano wakati wa kukusanya ushahidi kwenye uendeshaji mashauri ya rushwa ili kuisaidia Serikali katika mapambano dhidi ya Rushwa.

Kilindi. Watanzania wametakiwa kutoa ushirikiano katika mapambano dhidi ya rushwa ili kutokeza janga hilo katika jamii.

Wito huo umetolewa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2022, Sahili Geraruma wakati akizungumza na wananchi katika kijiji cha Msente wilayani Kilindi mkoani Tanga wakati wa makabidhiano ya Mwenge huo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Vijijini na Kilindi.

Amesema jamii inatakiwa kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha wanajitokeza kutoa ushahidi mahakamani wakati wa uendeshaji wa kesi za rushwa na kutoa taarifa za vitendo vya rushwa katika jamii zao.

Amesema kumekuwa na changamoto katika ukusanyaji wa ushahidi kwa kuwa watu wamekuwa hawajitokezi mahakamani kutoa ushahidi ili kukamilisha ushahidi.

"Tujitokeze kuisaidia Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa tutoe ushahidi mahakamani, pia tukatae kutoa na kupokea rushwa.

"Wananchi wana wajibu wa kuisaidia Serikali katika mapambano hayo ili kuweza kuijenga Tanzania imara yenye maendeleo," amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Abel Busalama amesema ukiwa wilayani Kilindi Mwenge utakimbizwa katika kata nane ambapo utazindua miradi nane ambayo ina thamani ya Sh634.5 milioni.

Amesema Mwenge wa Uhuru pia utatembelea Klabu ya Wapinga Rushwa katika Shule Wasichana ya Sekondari Kilindi iliyopo wilayani humo.

"Hapa kwetu Kilindi tunapambana na rushwa kwa kuhakikisha tunatoa elimu kuanzia ngazi ya shule za msingi ambapo kuna kuwa na klabu kama hii unayoiona wanapewa elimu kuhusu rushwa na madhara yake," amesema Mkuu huyo wa Wilaya.