Watatu mbaroni kwa kuua swala 28

Muktasari:

  • Watuhuwa hao walikutwa na nyara za serikali ambazo ni wanyamapori aina ya swala Thomson 28 wakiwa wamewaua.

Simiyu. Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu, linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kuua swala 28 na kukutwa na nyama ya swala hao katika makazi yao.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Agosti 18, 2023; Kamanda wa jeshi hilo Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe, amesema, kukamatwa kwa watu hao kunafuatia oparesheni iliyofanyika katika kijiji cha Mwasilimbi, wilayani Bariadi, Mkoa wa Simiyu.

Kamanda Swebe amewataja waliokamatwa kuwa ni pamoja na Masunga Madede (58), Mussa Masunga (28), na Yunis Makwaya (45), pamoja na pikipiki yenye usajili T 874 CUA ambayo ilikuwa inatumika kusafirishia nyara hizo za serikali.

"Watuhumiwa hawa walikutwa na nyara za Serikali ambazo ni wanyamapori aina ya swala 28, wakiwa wamewaua, watuhumiwa pamoja na vielelezo watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria," amesema RPC Swebe.

Akieleza mikakati ya kulinda wanyamapori katika pori la akiba Maswa, Ofisa Mhifadhi wa pori hilo Lawrence Okode, amesema mafanikio ya oparesheni hizo, hutokana na wao kupokea taarifa za siri na kuzifanyia kazi.

"Wanyama hao wana thamani ya Sh38 milioni, na hao wamewaua kwa matakwa yao binafsi, hivyo tunaendelea kuwatahadharisha wananchi wanaoishi maeneo yanayopakana na mapori yetu ya akiba kujiepusha na uwindaji usio wa kisheria,” amesema.