Watatu mbaroni tuhuma za mauaji Morogoro
Florenciana Edmund (38) enzi za uhai wake
Muktasari:
- Miongoni mwa wanaoshikiliwa ni mpiga debe katika stendi ya mabasi ya mjini Ifakara, Faraji Mwadanda (36) anatuhumiwa kumuua mke wake.
Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia mpiga debe katika stendi ya mabasi ya mjini Ifakara, Faraji Mwadanda (36) kwa tuhuma za kumuua mke wake aliyefahamika jina la Florenciana Edmund (38).
Florenciana ni mkatisha ushuru katika stendi hiyo, alifariki baada ya kudaiwa kumchoma na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema limetokea Julai 10, 2025 usiku baada ya kutokea ugomvi baina yao ambapo mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu mke wake kuwa na mahusiano ya mapenzi na wanaume wengine katika eneo hilo la stendi wanakofanyia kazi.
Kamanda Mkama amedai kuwa mtuhumiwa baada ya kufanya mauaji hayo aliutelekeza mwili wa mwanamke huyo ndani ya nyumba waliyokuwa wakiishi eneo la Kibaoni, hadi Julai 11 mwaka huu ulipogundulika.
"Baada ya ukimya na kutoonekana nje na hata kwenye eneo la kazi majirani zake walipata wasiwasi hivyo walitoa taarifa kwa serikali ya mtaa na polisi, ambapo baadaye ikibainika kuwa Florenciana ameuawa na mwili wake ulikuwa ndani," amesema Kamanda Mkama.
Amesema baada ya taarifa za mauaji hayo kufikishwa Polisi upelelezi ulianza ikiwa ni pamoja na kumtafuta mtuhumiwa ambapo alikamatwa kijiji cha Sakamaganga kata ya Siginal, akijiandaa kutoroka kwenda mkoani Arusha.
Kamanda Mkama amesema uchunguzi wa awali uliofanywa na Polisi umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi.
Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Bomani katika kata ya Kibaoni, James Hangahanga amesema tukio hilo limestua wananchi wengi wa mtaa huo kwani marehemu na mtuhumiwa walikuwa wakiishi jirani na eneo lao la kazi, ambapo ndio stendi kuu ya Ifakara.
Hangahanga amesema baada ya kupigiwa simu na majirani alifika eneo la tukio na kukuta wapangaji wengine wakilia na hivyo aliwasiliana na viongozi wenzake pamoja na Jeshi la Polisi na baadaye walipoingia ndani waliukuta mwili wa marehemu ukiwa umeloa damu.
"Inaonyesha kabla ya tukio la mauaji kulikuwa na ugomvi mkubwa na vuta nikuvute kwani baadhi ya vitu ndani vilikuwa vimevurugika na kudondoka chini, hata mtuhumiwa kufanya tukio hili kubwa la mauaji tena ya mke wake inashangaza sana. Mtuhumiwa alikuwa mtu wa watu na hakuwa na matukio ya ajabu, sijui kashindwaje kuwa na subira kwenye hili lililomsibu mpaka anachukua maamuzi haya," amesema Hangahang.
Amebainisha kuwa mazishi ya marehemu huyo yanafanyika leo Julai 14,2025 katika makaburi ya Lumemo na shughuli ya mazishi ilifanyika nyumbani kwa Kamonalelo mtaa wa Gavana Ndulu.
Katika tukio jingine Jeshi la Polisi limemkamata John Mayunga (34) mkulima kijiji cha Kitete kata ya Magole Wilaya ya Kilosa kwa tuhuma za mauaji ya Halifa Abdallah (19) ambaye ni dereva wa bodaboda, mkazi wa Kata ya Msowelo Wilaya ya Kilosa.
Kamanda Mkama amesema mauaji hayo yalitokea Julai 3 mwaka huu asubuhi eneo la Itete tarafa ya Magole Wilaya ya Kilosa.
Amesema Julai 2 mwaka huu mtuhumiwa alimkodi marehemu kutoka kijiji cha Msowelo kwenda kijiji cha Kife akiwa anaendesha pikipiki isiyokuwa na namba za usajili.
"Wakiwa njiani mtuhumiwa alimnyang'anya marehemu pikipiki hiyo na kumshambulia kwa silaha yenye makali na kumsababishia kifo, ambapo mtuhumiwa baada ya kufanya tukio hilo alitoroka na kuelekea mkoani Singida na akiwa eneo la Kitinku, Wilaya ya Manyoni mkoani Singida mtuhumiwa huyo aligongwa na kuumia sehemu mbalimbali za mwili," amesema Mkama.
Kamanda Mkama amesema kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata mtuhumiwa huyo alipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya matibabu na huko ndiko alikokamatwa na baadaye alisafirishwa hadi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kuendelea na kesi yake, huku akiendelea kupatiwa matibabu.
"Hata hivyo akiwa anaendelea na matibabu hali yake ilibadilika na kupewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu ambapo tumepokea taarifa kuwa amefariki dunia," amesema Kamanda Mkama.
Wakati huohuo Jeshi la Polisi limemkamata David Makamu (35) mkazi wa Chigela wilayani Gairo kwa tuhuma za kumuua Wilson Dastan (38) mjasiriamali mkazi wa Ukwamani wilayani Gairo kwa kumpiga na kitu butu wakati akiendesha pikipiki na kusababisha kupoteza uelekeo na kuanguka.
Kamanda Mkama amesema mauaji hayo yametokea Juni 23 mwaka huu usiku huko katika eneo la Kwakuta kijiji cha Ihenje kata ya Chigela wilayani Gairo, na baada ya kufanya tukio hilo mtuhumiwa alitoroka na kwenda kujificha kwa hawala yake eneo la Kata ya Sultan Manispaa ya Morogoro.
Matukio ya mauaji mkoani Morogoro yameendelea kushika kasi ambapo wiki mbili zilizopita mfanyabiashara ya maduka ya nyama aliuawa na kisha mwili wake kwenda kutupwa wilayani Handeni mkoani Tanga na pia mfanyabiashara wa miamala ya fedha naye aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa njiani kurudi nyumbani baada ya kufunga eneo lake la biashara.
Kufuatilia matukio hayo ya mauaji baadhi ya wananchi wa Morogoro wametoa maoni yao na kuwataka viongozi wa dini kuendelea kukemea vitendo hivyo kupitia nyumba za ibada.
Mmoja wa wananchi hao Mwanaidi Shoko amesema kuwa mauaji yaliyotokea katika kipindi hiki yanahusisha wivu wa mapenzi na ujambazi na tamaa ya kujipatia mali kwa nguvu.
"Sababu zote hizo za mauaji yanayotokea hapa Morogoro zimekatazwa na Mungu, hakuna sababu yoyote inayohalalisha mauaji, niwaombe viongozi wa dini hapa Morogoro kupitia misikiti na makanisa wakemee haya mauaji ambayo yanaelekea kutia doa mkoa wetu, pia vyombo vya sheria vichukue hatua na kutoa adhabu inayostahiki kwa wanaopatikana na hatua ili iwe fundisho," amesema Shoko.