Watatu wafariki kwa kushambuliwa na fisi

Muktasari:

  • Inaelezwa kuwa fisi hao wamezaliana na kuwa wengi hivyo chakula ambacho ni nyama pori hakiwatoshelezi, hivyo kuwinda binadamu na kuwashambulia kwa lengo la kutafuta chakula ili waishi.

Sengerema. Watu watatu wamefariki kwa kushambuliwa na fisi katika matukio tofauti wilayani Sengerema, mkoani Mwanza kati ya Januari hadi Februari 24, mwaka huu.

Tukio la kwanza lilitokea Januari 15, 2024, saa 12.30 jioni, kwa mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Nyakahako, Kata ya Chifunfu wilayani hapa, Sadiki Mashaka (16) kushambuliwa na fisi alipokuwa akichanja kuni mlimani.

Mwingine ni Mkazi wa Kijiji cha Lukumbi, Kata ya Chifunfu wilayani hapa, Mkabagobi Sibanga (70), aliyefariki dunia Januari 29, 2024, saa 11.30 alfajiri, baada ya kushambuliwa na fisi akielekea shambani kuvuna mahindi.

Katika tukio lingine, mtoto wa miaka sita, Adela Shimba, mkazi wa Kijiji cha Kafundokile, Kata ya Kasenyi wilayani humo aliuawa na fisi Februari 16, mwaka huu, alipokuwa ameambatana na bibi yake kwenda kuchota maji mtoni.

Taarifa za matukio hayo zimethibitishwa na Mkuu wa Idara ya Wanyamapori katika Halmashauri ya Sengerema, Paul Ponsian alipozungumza na Mwananchi.

"Kumekuwa na ongezeko la matukio ya fisi kushambulia wananchi, ndiyo maana tumeanza kuwasaka na kuwaua. Tunawaomba wananchi waendelee kutusaidia kutoa taarifa na ushirikiano ili tuwatokomeze wanyama hao,” amesema Ponsian.

Amesema kupitia misako iliyoendeshwa na maofisa wa Mamlaka ya Wanyamapori (Tawa) wilayani Sengerema, fisi watano wameuawa.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga amethibitisha ofisi yake kuwa na taarifa ya vifo hivyo, akiitaka jamii kuchukua tahadhari wanapokuwa maeneo yenye mapori.

“Tunawasisitiza wananchi kutotembea wakati wa usiku na kwenye maeneo ambayo wanyama hao wanaweza kuwa wanajificha,  wakati huu ambao Serikali inaendelea na msako wa kuwaua wanyama hao,” amesema Ngaga.

Diwani wa Chifunfu yalikotokea matukio mawili, Robert Madaha, amesema fisi hao si tu wameibua hofu, bali wanakwamisha shughuli za maendeleo.

“Ninawashukuru idara ya wanyamapori kuhakikisha wanawasaka na kuwaua fisi watano wanaodhaniwa kuwa ndiyo wamekuwa wakishambulia na kuua wananchi wa kata yangu,” amesema Madaha.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lukumbi, Kata ya Chifunfu, Chrizo Mtahoya amesema kwenye kijiji hicho ambako Mkabagobi alishambuliwa na kuuawa na fisi, ni tukio la nne katika kipindi cha miaka minne.

“Kuna ndugu yetu, Busemwa Rususu, alifariki 2017, Chausiku Shimo (2019) na mwanafunzi wa sekondari ya Chifunfu, Edward Ernest aliyeshambuliwa na kufariki mwaka 2023. Tunapata wakati mgumu kupambana na fisi hawa,” amesema.

Mkazi wa Chifunfu, Tizilahabi John ameiomba Serikali kuongeza jitihada za kuwatokomeza fisi hao ili kuimarisha usalama wa wananchi.

Sababu kushambulia wananchi

Ponsian alitaja changamoto ya ukosefu wa chakula porini na kwenye mapango wanamoishi kuwa moja ya sababu ya fisi hao kuvamia na kushambulia binadamu.

Amesema njia pekee ya kukabiliana nao ni kuwapunguza kwa kuwaua.

"Fisi hawa wanaonekana wameshazaliana na kuongezeka, hivyo hata chakula chao ambacho ni nyamapori hakitoshelezi matokeo yake hushambulia binadamu ili waweze kuishi," amesema Ponsian.