Watatu wajinyonga ndani ya siku tatu

Muktasari:

  • Wakazi wa Kijiji cha Makarwe wilayani Muleba wameingiwa hofu baada ya watu watatu kijinyonga ndani ya muda wa siku tatu kati ya Septemba 14 na 16.

Muleba. Wakazi wa Kijiji cha Makarwe wilayani Muleba wameingiwa hofu baada ya watu watatu kijinyonga ndani ya muda wa siku tatu kati ya Septemba 14 na 16.

Watu wawili wamepoteza maisha baada ya kujinyonga hadi kufa huku mmoja akiokolewa na mkewe aliyemkuta akiwa amening’inia juu ya mti akijinyonga.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Mwenyekiti wa Kijiji cha Makarwe, Wilson Charles alisema tukio la kwanza lilitokea Septemba 14, baada ya mkazi wa kijiji hicho, Godfrey Kaijage (53) kujinyonga hadi kufa.

Alisema kabla ya kujinyonga hadi kufa, marehemu Kaijage alishafanya mara tatu siku za nyuma lakini aliokolewa kabla hajapoteza maisha.

Alisema siku moja baada ya Kaijage kujinyonga, rafiki yake naye, Shedrack Joshua (36) naye alijinyonga muda mfupi baada ya kutoka kwenye mkesha wa msiba wa Kaijage.

“Tukiwa bado tunajiuliza kuhusu vifo vya marafiki hao wawili kujinyonga, kijana mwingine, Jackson Damian alikutwa akitaka kujiua kwa kujinyonga kabla ya kuokolewa na mke wake aliyemwona akiwa amening’inia juu ya mti jirani na nyumbani kwao,” alisema mwenyekiti huyo wa kijiji.

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi ambaye kwa sasa amehamishiwa makao makuu ya jeshi hilo jijini Dodoma alithibitisha kutokea kwa matukio hayo huku MKuu wa Wilaya Muleba, Toba Nguvila akiiambia Mwananchi kuwa amewaagiza askari polisi kuchunguzi chanzo cha matukio hayo yaliyoibua hofu miongoni mwa wananchi na kumchukulia hatua za kisheria Damian aliyenusurika kwenye jaribio lake la kutaka kujitoa uhai.

Nguvila pia ameziagiza kamati za amani za kijiji na kata wilayani hapa kuitisha vikao vya ndani na mikutano ya hadhara kujadili na kukemea matukio ya aina hiyo katika jamii kwa kila mwananchi kuwa mlinzi wa mwenzake.

Imeandikwa na Salvius Evarister na Anania Kajuni.