Watatu wanaswa na meno ya tembo Iringa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi akionesha silaha pamoja na meno ya tembo vipande yaliyokamatwa.

Muktasari:

Jeshi la Polisi Mkoani Iringa limewakamata watu watatu wakisafirisha meno  mawili ya tembo na vipande 17 yenye uzito wa kilo 69.5.

Iringa. Jeshi la Polisi Mkoani Iringa limewakamata watu watatu wakisafirisha meno  mawili ya tembo na vipande 17 yenye uzito wa kilo 69.5.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema watu hao wamekamatwa katika wilaya ya Mufindi Tarafa ya Ifwagi Mji wa Mafinga barabara kuu ya Iringa-Njombe.

Bukumbi amesema watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa wanasafirisha meno mazima mawili na vipande 17 pamoja na jino moja la kiboko kwa kutumia pikipiki.

“Watuhumiwa wote wamekamatwa wapo kituoni na tuliwakamata wakati askari polisi wakiwa doria baada ya kupata taarifa toka kwa raia wema, tunawaomba wananchi wazidi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kukomesha ujangili huo”amesema Bukumbi

Ofisa Mhifadhi Mwandamizi wa hifadhi ya Ruaha Mkoa wa Iringa, Sharif Abdul amesema matukio ya ujangili yamepungua lakini matukio haya ni kiashiria cha kuwa ujangili unarudi hususani ukiangalia idadi ya meno ya tembo 11 ambayo ni sawa na tembo 7.

“Hizi ni rasilimali za Watanzania nyara za Serikali hivyo tumepoteza kiwango kikubwa cha wanyama ambao ni kivutio cha watalii, kwa upande wa ujangili ni ishara kubwa kuwa ujangili unataka kurudi ama wale majangili waliokuwa wamejificha wanataka kurudi katika ulingo wa ujangili”