Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watayarishaji wa filamu wahamasishwa kugeukia utalii, uhifadhi

Muktasari:

  • Filamu hiyo inaelezea hatua kwa hatua kuhusu upandaji wa Mlima Kilimanjaro huku ikionyesha namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri theruji kwenye mlima huo ambao ni kivutio kikubwa cha utalii, ndani na nje ya nchi.

Dar es Salaam. Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Gervas Kasiga amewataka watayarishaji wa filamu nchini kuandaa filamu zinazotangaza vivutio vya utalii na kuhimiza utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kasiga ametoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati wa hafla ya uzinduzi wa filamu ya “Guardians of the Peak” iliyoandaliwa na Mtanzania, Ram Ally akishirikiana na Mtanzania mwenye asili ya China, Elizabeth Mrembo.

Filamu hiyo inaelezea hatua kwa hatua kuhusu upandaji wa Mlima Kilimanjaro huku ikionyesha namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri theruji kwenye mlima huo ambao ni kivutio kikubwa cha utalii, ndani na nje ya nchi.

Akizungumza baada ya kutazama filamu hiyo, Kasiga ambaye alimwakilisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, amewahimiza watayarishaji wa filamu kugeukia maudhui yanayoangazia utunzaji wa mazingira na kuhamasisha utalii.

“Tunawahimiza watayarishaji wa filamu kuona namna ya kutengeneza filamu za namna hii kwa sababu zinasaidia kuonyesha hali halisi ya maisha yetu ya kila siku na kusaidia kubadili tabia za wanajamii kutoka kwenye uhasi kuelekea kwenye tija,

Amewataka Watanzania kuwa na utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii na kukumbuka wajibu wao wa kulinda na kuhifadhi mazingira kwa manufaa yao ya sasa ya kwa manufaa ya vizazi vyao vijavyo.

“Unapotazama hii filamu, imebeba ajenda kwamba ndani yake tunakumbushwa ulinzi wa mazingira yetu, tunakumbushwa kulinda mlima wetu (Kilimanjaro) na kama mnavyofahamu, Mlima Kilimanjari ni mlima mrefu barani Afrika, lakini pia ni mlima mrefu uliosimama wima kuliko yote duniani,” amesema.

Amesisitiza kwamba ni muhimu kila mmoja akaangalia nafasi yake katika kutangaza vivutio vilivyopo, pia, kuongeza tija za maliasili za Tanzania na tija hizo hazitapatikana kama rasilimali hizo hazitalindwa.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, Nyakaho Mahemba amewapongeza watayarishaji wa filamu hiyo huku akiwakaribisha wasanii kwenda kuomba mikopo kwa ajili ya kazi zao.

“Tunatoa mikoa kwa wasanii ili kuwasaidia kuzalisha kazi bora zinazokidhi mahitaji ya soko la ndani pamoja na soko la nje. Tunatoa mikopo kuanzia Sh200,000 hadi Sh100 milioni kwa mtu mmoja mmoja, kikundi au kampuni, sharti utekeleze kazi za utamaduni au Sanaa.

“Riba zetu ni nafuu sana ambayo ni asilimia tisa inayotozwa katika salio la mkopo, kwa hiyo huduma kama hii huwezi kuipata popote, katika sekta yoyote, katika benki yoyote, katika nchi yoyote Zaidi ya Tanzania hususani sekta ya utamaduni na sanaa,” amesema.

Awali, mtayarishaji wa filamu hiyo, Ram Ally amesema wanakwenda kuonyesha kwamba kupitia sekta ya filamu wanaweza kufanya mambo makubwa tofauti na ilivyozoeleka, wamekuja na mbinu mpya za kuitangaza tasnia ya filamu kimataifa kupitia makala.

“Kupitia filamu hii, tutaweza kutangaza utalii katika soko la China na duniani kwa ujumla, na siyo tu kutangaza utalii, bali pia kuhamasisha uhifadhi wa mazingira. Sisi tumeona ni fursa ya kuitumia na tukalenga moja kwa moja kwenye Mlima Kilimanjaro kwa sababu unakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” amesema.

Ally amesema mradi huo ni wa miaka mitano na mwaka wa kwanza 2024, wamefanikiwa kuzindua filamu hiyo, mwaka huu watapanda tena Mlima Kilimanjaro wakibeba ajenda ya “Nishati Safi katika Mlima Kilimanjaro”.

“Tumekuwa tukibeba ajenda ya nishati safi kule mijini, lakini kule tukipeleka hii initiative kule kwenye vyanzo vya nishati ambavyo ni misitu, tutaweza kuilinda misitu yetu na kwa kufanya hivyo tutakuwa salama,” amesema Ally.

Naye Elizabeth amesema mradi huo ni muhimu kwa sababu unaelimisha utunzaji wa mazingira ili kwa nguvu ya pamoja watunze mazingira na mwishowe wanufaike na rasilimali zilizopo kwa miaka mingi ijayo.

“Tunaungana na wadau mbalimbali wa ndani na nje kwa ajili ya kujenga taifa la Tanzania,” amesema Elizabeth na kuuongeza kuwa filamu hiyo itachochea soko la utalii nchini China na kuendeleza uhusiano na taifa hilo.