Wateja benki ya FBME walipwa Sh2.42 bilioni
Muktasari:
- Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mwanaidi Ali Khamis amesema Sh2.42 bilioni zimelipwa kwa wateja wenye amana katika benki ya FBME sawa na asilimia 52.13 ya Sh4.65 bilioni zinazotakiwa kulipwa kwa wateja hao.
Dodoma. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mwanaidi Ali Khamis amesema Sh2.42 bilioni zimelipwa kwa wateja wenye amana katika benki ya FBME sawa na asilimia 52.13 ya Sh4.65 bilioni zinazotakiwa kulipwa kwa wateja hao.
Ameeleza hayo leo Jumatano Februari 3, 2021 bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Jang'ombe (CCM) Ali Hassan King.
"Serikali imefikia hatua gani katika kufuatilia fedha za wananchi zilizopo katika benki ambazo zimezuiwa kuendesha shughuli zao nchini,” amehoji King.
Akijibu swali hilo, Mwanaidi amesema mwaka 2017 na 2018 Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilizifutia leseni ya kufanya biashara ya kibenki benki saba kwa mujibu wa vifungu vya sheria ya mabenki na taasisi za fedha ya mwaka 2006.
Amezitaja benki zilizofutiwa leseni ya kufanya biashara nchini ni pamoja na FBME Bank Ltd, Mbinga Community Bank Plc, Njombe Community Bank Ltd, Kagera Farmers’ Cooperative Bank Ltd, Meru Community Bank Ltd, Efatha Bank Ltd na Covenant Bank for Women (T) Limited.
Amesema baada ya kuzifutia leseni benki hizo, BoT iliiteua bodi ya bima ya Amana (Deposit Insurance Board –DIB) kuwa mfilisi.
Amebainisha kuwa katika kutimiza wajibu wake wa msingi kisheria, bodi ya bima ya Amana ilianza shughuli ya kulipa fidia ya bima ya amana ya hadi Sh1.5 milioni kwa waliostahili kulipwa bima katika Benki hizo na shughuli hiyo bado linaendelea kwa wateja ambao hawajajitokeza kuchukua fidia.
Amesema sanjari na zoezi hilo, DIB inaendelea na kazi ya ufilisi wa benki hizo.
"Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba 2020 jumla ya Sh4.94 bilioni zimeshalipwa kwa wateja wenye amana wa benki sita za wananchi (Community Banks) kama zilivyotajwa hapo juu ukiiondoa Benki ya FBME," amesema.
Amesema malipo hayo ni sawa na asilimia 77.27 ya kiasi cha Sh6.39 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya kulipa fidia.
Mwanaidi amesema wateja waliolipwa ni 21,675 kati ya wateja 57,076 ikiwa ni asilimia 37.98 ya wateja waliokuwa na amana zilizostahili fidia.
Kuhusu Benki ya FBME, Mwanaidi amesema hadi mwishoni mwa Desemba 2020, Sh2.42 bilioni zimelipwa kwa wateja wenye amana ambazo ni sawa na asilimia 52.13 ya kiasi cha Sh4.65 bilioni.
Amesema wateja waliolipwa ni 3,443 kati ya wateja 6,628 ambao ni sawa na asilimia 51.95 ya wateja waliokuwa na amana zilizostahili fidia.
Amesema wateja waliokuwa na amana inayozidi Sh1.5 milioni watalipwa kiasi kilichobakia chini ya kazi ya ufilisi ambapo kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufilisi kiasi kitakacholipwa kitategemea fedha zitakazopatikana kutokana na kuuza mali za Benki husika.
Amesema ukusanyaji madeni na mali za benki hizo linaendelea ili kupata fedha za kuwalipa wateja wenye amana za zaidi ya Sh1.5 milioni.