Watendaji wa ardhi wamchefua RC
Muktasari:
- Watendaji wa Idara ya Ardhi katika wilaya zote za Mkoa wa Songwe wamenyoshewa kidole kwa utendaji usioridhisha katika kutekeleza majukumu yao, yakiwamo ya ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali na utoaji wa hatimiliki za ardhi na makazi.
Songwe. Watendaji wa Idara ya Ardhi katika wilaya zote za Mkoa wa Songwe wamenyoshewa kidole kwa utendaji usioridhisha katika kutekeleza majukumu yao, yakiwamo ya ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali na utoaji wa hatimiliki za ardhi na makazi.
Akifungua kikao cha kazi, Mkuu wa Mkoa Songwe Omary Mgumba amesema ofisi yake haijaridhishwa na kazi ya maofisa hao kufuatia taarifa iliyotolewa na Kamishina wa Ardhi ambayo inaonesha idara ya ardhi haikufanya vizuri katika kukusanya mapato na usajili wa hati na upimaji.
Amesema idara ya ardhi pekee ndiyo imeuangusha mkoa katika ukusanyaji mapato ikilinganisha na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na halmashauri za wilaya ambazo zinaendelea kufanya vizuri na kuubeba Mkoa kitaifa kwa ukusanyaji mapato.
Awali akiwasilisha taarifa katika kikao hicho Kamishina wa Ardhi, Suma Mwakasitu amebainisha kuwa idara hiyo haijafanya vizuri katika ukusanyaji maduhuri ya Serikali, utoaji wa hati na urasimishaji ardhi.
Amesema halmashauri zote hazijafanya vizuri katika robo ya kwanza ya mwaka huu, na kuwa hii ndiyo sababu ya kuitisha mafunzo hayo ili kukumbushana wajibu wa kila mmoja na kuweka malengo na mikakati mipya ya utendaji kadi.
Wataalamu wa sekta ya ardhi mkoani Songwe wameanza mafunzo ya siku tatu ambayo yatawawezesha kupokea na kukumbushana masuala mbalimbali yahusuyo sekta hiyo.