WaterAid, NEMC waungana kuimarisha huduma za maji na usafi wa mazingira
Mkurugenzi wa WaterAid Tanznaia Anna Mzinga na Mkurugenzi Mtendaji wa NEMC Dk Immaculate Semesi wakionyesha hati ya makubaliano.
Muktasari:
- Kupitia ushirikiano huo, taasisi hizo mbili zitashirikiana katika upangaji wa shughuli, utoaji wa msaada wa kitaalamu, usimamizi wa pamoja wa miradi pamoja na uhamasishaji wa rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Wash.
Dar es Salaam. Katika hatua inayotarajiwa kuimarisha upatikanaji endelevu wa maji safi na huduma za usafi wa mazingira nchini, WaterAid Tanzania na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) zimesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) kwa lengo la kuunganisha nguvu katika kulinda mazingira na vyanzo vya maji.
Makubaliano hayo yanakusudia kuendeleza programu za maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi (WASH) zinazozingatia ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza leo wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Mkurugenzi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga, amesema upatikanaji wa maji safi na salama hauwezi kutenganishwa na ulinzi wa mazingira pamoja na usimamizi endelevu wa rasilimali asili.
“Ni heshima kushirikiana na taasisi yenye jukumu muhimu la kulinda mazingira ya Tanzania, jambo ambalo linaendana moja kwa moja na dhamira yetu ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za maji na usafi wa mazingira,” amesema Mzinga.
Amesema mifumo ikolojia inayosimamiwa vizuri pamoja na huduma za maji zinazostahimili athari za tabianchi ni msingi muhimu wa kuhakikisha miradi ya maji na usafi wa mazingira inadumu kwa muda mrefu.
Kupitia ushirikiano huo, taasisi hizo mbili zitashirikiana katika upangaji wa shughuli, utoaji wa msaada wa kitaalamu, usimamizi wa pamoja wa miradi pamoja na uhamasishaji wa rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya WASH.
Aidha, zitaanzisha majukwaa ya kubadilishana uzoefu na maarifa kwa wadau wa sekta ya maji na usafi wa mazingira huku zikisisitiza uzingatiaji wa sheria za mazingira na viwango vya ubora wa huduma nchini.
Shirika la WaterAid Tanzania, tayari limewezesha zaidi ya watu milioni 1.9 kupata maji safi na salama, huku zaidi ya watu 790,000 wakinufaika na huduma bora za usafi wa mazingira.
Pia zaidi ya watu milioni 4.3 wamefikiwa kupitia afua mbalimbali za usafi binafsi katika maeneo tofauti nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi amesema ushirikiano huo umekuja wakati muhimu ambapo mahitaji ya kulinda vyanzo vya maji na mazingira yanaongezeka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema moja ya rasilimali muhimu inayosimamiwa na NEMC ni maji, hivyo ushirikiano huo utaimarisha juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwa njia endelevu.
“Makubaliano haya ni hatua muhimu kwa taasisi hizi mbili kurasimisha ushirikiano utakaosaidia kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha huduma za maji zinaendelea kuwa salama na endelevu kwa wananchi,” amesema Dk Semesi.
Ameongeza kuwa NEMC itaendelea kusimamia tathmini za mazingira katika maeneo ya utekelezaji wa miradi ya maji, kufuatilia viwango vya ubora wa maji pamoja na kuhakikisha sheria na kanuni za mazingira zinazingatiwa.
Kwa mujibu wa Dk Semesi, ushirikiano huo pia utaisaidia NEMC kupata taarifa, takwimu na utaalamu muhimu utakaosaidia kuimarisha uhifadhi wa mazingira na usimamizi wa rasilimali za maji nchini.