Watofautiana nyimbo za kisasa kuchangia kuporomoka maadili

Muktasari:

  • Mjadala wa Mwananchi X-Space wenye mada isemayo ‘Je maudhui ya muziki wa sasa huchangia mmomonyoko wa maadili?’ na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) umeibua mitizamo tofauti juu ya nyimbo za kisasa kuchangia mmomonyoko wa maadili.

Dar es Salaam. Mhariri wa Jarida la Burudani gazeti la Mwananchi Kalunde Jamal amewaomba wasanii wakiihurumie kizazi kijacho kutokana na aina ya nyimbo wanazotoa kuchangia mmomonyoko wa maadili.

Kalunde amesema hayo leo Jumatano, Novemba 22, 2023 kwenye mjadala wa Mwananchi X-Space wakati akichokoza mada isemayo ‘Je maudhui ya muziki wa sasa huchangia mmomonyoko wa maadili?’

Mjadala huo umeandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) na kushirikisha wadau mbalimbali.

Kalunde amesema muziki wa kizazi kipya kwa sasa unachangia mmomonyoko wa maadili, akitolea mfano siku alipopanda kwenye daladala akamsikia mwanafunzi akiimba wimbo usio na maadili wenzake wakimuonya kuachana na wimbo huo lakini mtoto huyo aliendelea kuuimba.

“Wasanii wakihurumie kizazi kijacho kutokana na nyimbo wanazotoa kutokuwa na maadili,” amesema

Kalunde amesema licha ya hatua zinazochukuliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kuzifungia nyimbo zisizo na maadili bado nyimbo nyingi zinaendelea kutolewa kila uchwao.

“Katika nyimbo 10,000 ukifungia moja ni sawa na kazi bure kwasababu zinaimbwa nyimbo nyingi, tasnia tunapoelekea ni shida kama tunataka kukuza hii tasnia turudi kwenye misingi yetu tutumie maneno mazuri yenye kuijenga jamii kwenye nyimbo,” amesema

Kwa upande wake, muandaaji wa maudhui ya burudani, Blessed Tillah akichangia mada hiyo amewataka wadau mbalimbali wa muziki kuepuka kunyoosheana vidole.

“Mashabiki wanasema wasanii hawaimbi nyimbo za maadili na wasanii wenyewe wanasema wanaangalia nyimbo zinazopendwa na mashabiki.

“Sisi wadau wa muziki na vyombo vya habari tunanyooshewa vidole kwamba tunazicheza nyimbo hizo lakini ukiangalia hizo nyimbo ndizo zinazoombwa na mashabiki, hata kwenye kumbi za muziki hizi nyimbo zinazolalamikiwa ndizo zinapigwa,” amesema na kuongeza:

“Tukubali sote kwamba kuna sehemu tumefeli sehemu fulani kwenye maadili.”

Hata hivyo, Meneja wa Muziki, Frank Johnson anadhani suala la mmomonyoko wa maadili halijaanzia kwenye muziki bali kwenye familia.

Johnson amesema kama muziki wa ndani unachangia mmomonyoko wa maadili hata muziki wa nje nao una mchango mkubwa lakini hatua zozote ambazo zimechukuliwa kuzuia nyimbo hizo kuingia nchini.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Meneja wa Muziki, Frank Mkuvielwa ambaye amesema mwanamuziki hawezi kufanya kitu ambacho hakina mashiko kwa walaji.

“Jamii inafurahishwa na mambo ambayo si ya maadili kwasababu jamii inapenda wasanii wanalazimika kuimba, mziki ni sehemu ndogo ya maadili tunayoipigania, tuna kazi kubwa ya kufanya kwenye nyumba zetu za ibada na kwenye jamii,” amesema

Kwa upande wake, mdau mwingine wa muziki aliyejitambulisha kwa jina la Abddalah amesema tatizo lililopo ni wasanii kutojua wanatengeneza muziki kwa ajili gani.

“Jamii inakataa elimu kwenye muziki bali inahitaji burudani zaidi, muziki ni sehemu ndogo inayosababisha mmmomonyoko wa maadili,” amesema

Naye Mchangia mada kwenye mjadala huo, Clay Mwaifwani amepinga dhana ya kuwa muziki wa sasa unachangia kwenye mmomonyoko wa maadili.

Amesema jamii kwa ujumla imepoteza maadili yake. Kupitia wasanii jamii inaona mitizamo na falsafa zinazoongoza maisha ya jamii.

“Kwa kipindi hiki si jambo la kushangaza kuona mtoto wa kike anasema anaishi kwa kutegemea kuhongwa fedha na wanaume. Hivyo kwenye muziki wasanii wa kike wanabeba maudhui hayo kuyaimba,” amesema

“Mtu haoni haya kusema yeye ni mlevi, zamani ulevi ilikuwa ni jambo la aibu lakini sasahivi anaweza kusema yeye ni mlevi na anainuka kushangilia,” amesema

Amesema mwanamuziki anaimba kilichopo kwenye jamii na jamii inafurahishwa na mambo ambayo sio maadili. Amesema msanii kwa sasa hawezi kuimba masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Amesema sisi kwenye jamii ndio walaji na mwanamziki hawezi kuimba kitu hakina mashiko kwa walaji. Hivyo wanalazimika kuimba kitu ambacho jamii itakipokea.