Watoto mkoani Dodoma, Tabora waongoza kuanza ngono chini ya miaka 15
Muktasari:
- Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (Tacaids) imesema Mkoa wa Dodoma na Tabora inaongoza kwa kuwa na asilimia kubwa ya vijana chini ya umri wa miaka 15 wanaojihusisha ngono.
Dodoma. Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (Tacaids) imesema Mkoa wa Dodoma na Tabora inaongoza kwa kuwa na asilimia kubwa ya vijana chini ya umri wa miaka 15 wanaojihusisha ngono.
Mratibu wa programu ya ongea wa tume hiyo, Dk Pendo Saro ameyasema hayo leo Jumamosi Septemba 11, 2021 wakati wa uzinduzi wa programu hiyo inayolenga kutoa elimu kwa vijana kupitia vipindi vya radio.
Dk Pendo amesema takwimu zinaonyesha kuwa vijana kati ya umri wa miaka 10 hadi 19 nchini ni zaidi milioni 12 na walio na umri wa kati ya miaka 15 hadi 19 ni milioni 5.6.
Amesema tafiti mbali zilifanyika kuangalia hali halisi ya vijana katika masuala ya afya ya uzazi ziliangalia pia eneo la tabia za kingono.
Amesema katika tafiti iliyofanyika mwaka 2016/ 2017 ilionyesha vijana kati ya miaka 15 hadi 24 wanajihusisha ngono ikilinganishwa na watu wazima.
Amesema asilimia 14 ya vijana wa kiume Tanzania na asilimia tisa ya wa kike wanajihusisha na ngono kabla hawajafika umri wa miaka 15 huku asilimia 21.6 ya vijana wakibainika kutokuwa na elimu yoyote kuhusu afya ya uzazi na Ukimwi.
Amesema kuwa utafiti huo ilionekana kuwa kwa kadri vijana wanavyopata elimu idadi ya wanaoshiriki ngono wakiwa na umri mdogo ilikuwa ikipungua.
Dk Pendo amesema kuna mikoa ilionyesha kuwa na hali mbaya zaidi ikiwemo Dodoma ambao asilimia 22 ya vijana walionekana kujihusisha na ngono katika umri wa chini ya miaka 15.
Amesema Mkoa wa Dodoma unafuatiwa na Mkoa wa Tabora ambao asilimia 20 ya watoto walikuwa wakijihusisha na ngono kwenye umri huo.
Mkoa wa Iringa ulionekana kutokuwa na hali mbaya kwa kuwa na asilimia 4.9 ya watoto wanaojihusisha na ngono.
Akizindua program hiyo, naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Ummy Ndeliananga amewataka vijana kufuatilia programu mbalimbali na maudhui ya afya ya uzazi yatakayowezesha kufanya maamuzi sahihi ili waweze kufikia ndoto zao.
Amesema tafiti zinaonyesha vijana wakipewa taarifa na elimu ya kukabiliana na mazingira yaliyopo wanaweza kupata huduma rafiki na kujenga uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha yao na kupunguza tabia hatarishi.