Watoto wasiobalehe kushindanishwa usomaji Quran
Mratibu wa mashindano, ya usomaji wa Qur'an Sauti za Dhahabu, Abubakar Ali, wapili kutoka kushoto akizungumza na Vyombo vya Habari namna yatakayokuwa
Muktasari:
- Mashindano hayo yanayowahusisha watoto wa kike na wa kiume ambao hawajabalehe yamezinduliwa rasmi mkoani Dar es Salaam huku wazazi wakihimizwa kuwaandikisha watoto wao wenye uwezo wa kusoma Quran kwa kuzingatia tajwid na matamshi sahihi.
Dar es Salaam. Wakati mijadala ya matumizi ya teknolojia na mitandao ya kijamii yakitajwa kuongeza changamoto za maadili kwa watoto, waandaaji wa mashindano ya usomaji wa Quran ‘Sauti za Dhahabu’ wamesema wameanzisha jukwaa hilo kwa lengo la kujenga kizazi chenye maadili mema kupitia elimu ya dini.
Mashindano hayo yanayowahusisha watoto wa kike na wa kiume ambao hawajabalehe yamezinduliwa rasmi mkoani Dar es Salaam huku wazazi wakihimizwa kuwaandikisha watoto wao wenye uwezo wa kusoma Quran kwa kuzingatia tajwid na matamshi sahihi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo, Dar es Salaam leo Jumapili, Julai 26, 2026, mratibu wa mashindano hayo, Abubakar Ali amesema wazo la kuanzisha limetokana na hitaji la kuwajenga watoto katika misingi ya dini kabla hawajaathiriwa na changamoto zinazotokana na mazingira ya sasa.
"Tunataka kujenga kizazi kinachomjua Mwenyezi Mungu tangu utotoni. Mtoto akijengewa msingi mzuri wa Quran akiwa mdogo, anakuwa na nafasi kubwa ya kukua katika maadili mema," amesema.
Kwa mujibu wa Ali, mashindano hayo yaliyoandaliwa na Africa TV yataanza Agosti Mosi jijini Dar es Salaam kabla ya kusambaa katika mikoa mingine nchini na yanatarajiwa kufanyika kwa muda wa mwezi mmoja kabla ya kufikia hatua ya fainali.
Amesema lengo la mashindano hayo ni kuibua, kutambua na kuendeleza vipaji vya usomaji wa Quran Tukufu kwa kuzingatia tajwid, matamshi sahihi na sauti nzuri, sambamba na kuwalea watoto katika maadili mema.
Amesema jumla ya Sh10 milioni zimetengwa kwa ajili ya washindi watatu wa juu. Mshindi wa kwanza atazawadiwa Sh5 milioni, wa pili Sh3 milioni na wa tatu Sh2 milioni.
"Tumeamua kuandaa mashindano haya tukijikita zaidi katika sauti nzuri na usomaji unaozingatia matamshi sahihi. Tunataka kutengeneza kizazi kinachoujua Quran tangu utotoni. Kwa kuwa huu ni msimu wa kwanza, tutaanzia Dar es Salaam," amesema.
Ali amesema mashindano hayo yataendeshwa kwa mfumo unaofanana na Quran Star Search, yakisimamiwa na jopo la majaji saba watakaotathmini washiriki na kuwachagua wanaostahili kusonga mbele.
Amefafanua mashindano hayo yatakuwa na hatua nne na yatafanyika katika misikiti mitano jijini Dar es Salaam, ikiwemo Msikiti wa Kichangani uliopo Magomeni. Watoto wote wa Kiislamu wanaruhusiwa kushiriki kupitia shule zao.
"Kuanzia Agosti Mosi tutaanzia Msikiti wa Kichangani ambapo watoto kutoka wilaya za Ubungo na Kinondoni watakusanyika kwa hatua ya awali ya usaili utakaokuwa ukifanyika kila siku za Jumamosi na Jumapili na kurushwa mubashara kupitia kituo cha Africa TV," amesema.
Ameitaja misikiti mingine itakayotumika ni pamoja na Msikiti wa Taqwa (Ilala) na Msikiti wa Bakhresa. Katika hatua ya kwanza, majaji watachagua watoto 70 watakaoingia hatua inayofuata, ambapo watachujwa na kubaki washiriki 30.
Baada ya hapo, washiriki hao 30 wataendelea kushindanishwa hadi kupatikane washindi sita bora watakaoingia hatua ya fainali. Kisha kupatikana washindi watatu bora watakaogawana zawadi ya Sh10 milioni.
Ofisa Masoko wa kituo hicho, Rajabu Msami, amesema ingawa kuna mashindano mengi yanayofanyika nchini, wao wameona umuhimu wa kuwekeza katika kundi la watoto wasiobalehe kutokana na changamoto za maadili zinazolikabili.
"Tumeona haja ya kugusa eneo hili la watoto wadogo ambao hawajabalehe. Tunataka wajifunze kusoma Quran kwa kuzingatia sheria zake, ndiyo maana tumeandaa mashindano haya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo shule za msingi za Kiislamu nchini," amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Nurdin Kishki, amesema mashindano hayo yanawahusu watoto wote wa kike na wa kiume, mradi wawe hawajabalehe.
Amesema mashindano hayo hayalengi kuhifadhi Quran bali yanazingatia uwezo wa kusoma kwa tajwid sahihi na sauti nzuri kwa mujibu wa sheria za usomaji wa Qur'an.
Mwakilishi wa jopo la majaji saba, Sheikh Ali Asaa, amesema wamepewa dhamana kubwa ya kuhakikisha ushindani unazingatia haki na kanuni zote za usomaji wa Quran.
Amesema mashindano hayo ni hatua muhimu ya kuwahamasisha watoto kujifunza Quran na kupunguza athari zinazotokana na matumizi mabaya ya teknolojia na simu za mkononi.
"Bila kuwekeza katika malezi ya Quran hatuwezi kuwa na kesho bora kwa watoto wetu. Mageuzi ya aina hii yanahitajika ili kuwahamasisha watoto kuisoma, kuielewa na kuishi kwa kuzingatia mafundisho yake," amesema.