Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watu 10 kortini Sumbawanga kwa makosa ya uhaini, kutaka kuzuia uchaguzi

Watuhumiwa wa kosa la uhaini wakiingia mahakamani kwa ajili ya kusomewa mashitaka yanayowakabili. Picha na Neema Mtuka

Muktasari:

  • Washitakiwa hao wamepandishwa kizimbani jana Novemba 10, 2025 na kusomewa mashitaka mawili ya kesi namba PI 16146 /2025.

Sumbawanga. Watu 10 katika Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sumbawanga kwa kosa la uhaini na kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, makosa ambayo wanatuhumiwa kuyafanya kati ya Machi na Oktoba 30, 2025.

Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa Serikali, David Mwakibolwa amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Grace  Mafuta (42), Samson Noel (25), Isack Myamba (24) na Frank Nyansio (42).

Wengine ni Filbert Malela (29), Erenest Kanoni (24), Meshack Mwambinga (25), Alfred Bendera (22), Boniface Kalezu (30) na Daud Machelela (22).

Washtakiwa hao wamepandishwa kizimbani jana Novemba 10, 2025 na kusomewa mashtaka mawili ya kesi namba PI 16146 /2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sumbawanga, Kisasila Saguda.

Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa Serikali David Mwakibolwa amesema kosa la kwanza ni kuwa kwa nyakati tofauti kati ya Machi na Oktoba 30, 2025 katika maeneo tofauti ndani ya Mkoa wa Rukwa walikula njama na kutenda kosa la uhaini chini ya kifungu namba 384 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai marejeo ya kifungu cha 16 cha mwaka 2023.

Katika kosa la pili, amesema washtakiwa hao walitenda kosa la uhaini chini ya kifungu cha 39 (2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, sura ya 16, marejeo ya mwaka 2023. Ambapo maelezo ya kosa ni kuwa washtakiwa hao, Oktoba 30, 2025 katika mji wa Sumbawanga walikuwa na nia ya kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025.

Pia, waliitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kujiingiza kufanya fujo na kusababisha uharibifu wa mali za Serikali zinazotumika kutolea huduma muhimu.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sumbawanga, Kisasila Saguda amewataka washtakiwa hao kutojibu chochote hadi hapo shauri hilo litakapokwenda kusikilizwa Mahakama Kuu.

Upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na makosa waliyoshtakiwa nayo yote hayana dhamana hivyo  wamerudishwa mahabusu hadi Novemba 24, 2025, kesi itakapotajwa tena.