Watu 10 wafa ajalini wilayani Same

Muktasari:

  • Watu 10 wamefariki  katika ajali ya gari iliyotokea kijiji cha Kirinjiko Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Moshi/Same. Watu 10 wamefariki  katika ajali ya gari iliyotokea kijiji cha Kirinjiko Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Baadhi ya waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea leo jioni Jumanne Aprili 13, 2021  baada ya gari aina ya Toyota Alphard kugongana uso kwa uso na gari jingine aina ya Toyota Noah,  ni waombolezaji waliokuwa wakitoka mkoani Arusha kwenda Lushoto mkoani Tanga.

Awali Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Amon Kakwale aliieleza Mwananchi Digital kuwa watu sita walikufa papo hapo lakini taarifa zilizomkariri mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule zinaeleza kuwa idadi ya waliokufa ni 10 na majeruhi ni 12.

Amesema abiria waliokuwamo katika Alphard walikuwa wakitokea Arusha kwenda Lushoto kwenye msiba na kwamba Noah ilikuwa ikitoka Hedaru kwenda Same.

 “Alphard ilipata tyre bust (kupasuka gurudumu) ya nyuma ikayumba ikaenda kugongana na hiyo Hiace na wamekufa watu 10 na majeruhi 12. Watu 12 waliojeruhiwa walipelekwa hospitali ya wilaya ya Same.”

 “Majeruhi watano wakawa na hali mbaya ikabidi wapelekwe KCMC.  Hapa kwetu  wamebaki watu saba ambao wanaendelea kupatiwa matibabu. Miili minne imetambuliwa na sita ndugu zao walikuwa wanaendelea  kutafutwa,” amesema.