Watu 115 kusafisha damu Bugando kila wiki kuokoa figo

Wakazi wa Mwanza wakiwa kwenye foleni kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya magonjwa ya figo katika hospitali ya Bugando ikiwa ni maadhimisho ya siku ya figo duniani yaliyofanyika leo hospitalini hapo. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Watu 115 wanapatiwa huduma ya kusafisha damu kutokana na matatizo ya figo katika hospitali ya Bugando huku wagonjwa 600 wakitibiwa katika kliniki ya magonjwa hayo kwa mwezi.

Mwanza. Wakati dunia ikiadhimisha 'Siku ya Figo' Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando imesema watu 115 wanapatiwa huduma ya kusafisha damu (Dialysis) kutokana matatizo ya figo kila wiki.

Mbali na wanaofanyiwa Dialysis, Daktari bingwa bobezi wa magonjwa ya figo, Said Kanenda pia amesema wagonjwa 150 wanapatiwa matibabu katika kliniki ya magonjwa ya figo kila wiki sawa na wagonjwa 600 kwa mwezi.

Akizungumza Machi 9, 2023 kwenye shughuli ya upimaji wa magonjwa ya figo bila malipo iliyofanyika hospitalini hapo, Dk Kanenda amesema kati ya wagonjwa wanaopatiwa huduma ya kusafisha damu wagonjwa zaidi ya 28 wanahitaji huduma ya upandikizaji wa figo huku wengi wao wakiwa na umri chini ya miaka 65.

"Wagonjwa hawa tunawahudumia kwenye kliniki yetu ya magonjwa ya figo inayofanyika kila Jumatatu. Baadhi yao ni wale ambao ugonjwa haujafika hatua mbaya ya kuhitaji kusafishwa damu (Dialysis)," amesema Dk Kanenda

Daktari huyo ametaja baadhi ya tabia zinazochangia matatizo ya figo kuwa ni matumizi holela ya dawa (antibiotics), ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu, uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe kupindukia.

Pia, amesema tafiti zinaonyesha asilimia saba ya wakazi wa maeneo ya vijijini wana dalili za ugonjwa wa figo na mjini asilimia 13 huku mfumo wa maisha kwa wakazi wa maeneo ya mjini ukitajwa kuchangia ongezeko hilo.

Amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya ya figo zao mapema kuepuka changamoto ya kugundua ugonjwa wa figo katika hatua mbaya huku akidokeza kuwa huduma ya kusafisha damu inagharimu hadi Sh300,000.

"Kwa mgonjwa ambaye figo zake zimeathirika sana, anatakiwa kufanyiwa Dialysis mara tatu au nne kwa wiki sasa matibabu haya ni gharama sana kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla ndiyo maana tunasisitiza watu pia wajiunge na Bima ya Afya," amesema

Mbali na hilo, Dk Kanenda amesema huduma ya upandikizaji wa figo inayotolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na hospitali ya Benjamin Mkapa itaanza kutolewa Bugando kuanzia mwaka 2024 huku akiwasisitiza wananchi kuepuka tabia zinazohatarisha usalama wa figo zao.

Mkazi wa Bugarika jijini Mwanza, Beka Mgarya amesema matumizi holela ya dawa yamechangia figo zake kupata hitilafu huku akiwataka wananchi kuepuka matumizi holela ya dawa za tiba na dawa za asili.

"Nashukuru naendelea na matibabu, leo nimekuja kupima hapa inaonekana afya ya figo zangu imeanza kuimarika. Wana jamii wajenge utamaduni wa kupima afya mara kwa mara kubaini hali zao," amesema

Naye, Rita Rweyemamu ameiomba Bugando kutanua wigo wa huduma ya upimaji wa magonjwa ya figo bila malipo kwa wakazi wa maeneo ya vijijini ili kuongeza utambuzi wa visa vipya vya watu waliohatarini kufariki kwa magonjwa ya figo bila kutambua.