Watu 12 wafariki kwa kugonga treni kwa miaka miwili

Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Zakaria Mwansasu (kulia mwenye kipaza sauti) akizungumza na viongozi wa Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (Latra) alipotembelea banda la taasisi hiyo wakati wa maadhimisho ya wiki ya Usalama wa Reli yanayofanyika Kitaifa mjini Tabora. Picha na Robert Kakwesi

Muktasari:

Ndani kipindi hicho, jumla ya matukio 42 ya vyombo vya moto yakiwemo magari madogo, mabasi na pikipiki kugonga treni yaliripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Tabora. Watu 12 wamefariki dunia kwa kugonga treni katika matukio tofauti yaliyotokea kati ya Juni, 2021 hadi Juni, 2023.

Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Reli Shirika la Reli Tanzania (TRC), Nelson Ntejo amesema ndani kipindi hicho, jumla ya matukio 42 ya vyombo vya moto yakiwemo magari madogo, mabasi na pikipiki yaliripotiwa kugonga treni katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza mjini Tabora yanakofanyika maadhimisho ya kitaifa ya wiki ya usalama wa reli, Ntejo amesema watu watu sita waliogonga treni katika njia ya Dar es salaam-Dodoma, wakati watu wengine watatu waligonga treni katika njia ya Dodoma-Tabora.

Amesema watu wawili waligonga treni katika njia ya Tabora huku mtu mmoja akiripotiwa kugonga treni katika njia ya Tanga-Arusha.

‘’Ndani ya kipindi hicho, watu 18 walikutwa wamefariki kwenye njia ya reli huku sababu za vifo vyao vikiwa havijulikani,’’ amesema Ntejo

Katika matukio mengine, Ntejo amesema watu wawili walifariki baa ya kuruka kutoka kwenye Treni huku mtu mmoja alianguka kutoka kwenye Treni.

Amesema licha ya jitihada za elimu kwa umma, hali ya usalama katika njia ya reli bado siyo ya kuridhisha na uongozi wa TRC unaendelea na kampeni ya elimu kwa umma kupitia njia na majukwaa tofauti ikiwemo taasisi za elimu, mikutano, vipindi vya redio na televisheni na maadhimisho mbalimbali.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli nchini (TRC), Masanja Kadogosa amesema shirika hilo litaendelea kutekeleza kampeni ya elimu kwa umma kuanzia kwa wanafunzi wa shule za msingi kuwezesha jamii kujua sheria na kanuni za usalama wa reli.

Kupitia salamu zake zilizosomwa na Mkuu wa Chuo cha Teknolojia ya Reli, Damas Mwajanga, Kagogosa amesema ufahamu wa jamii kuhusu usalama wa reli ni msingi muhimu katika ulinzi na usalama wa reli.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian amewataka madereva kuacha jeuri ya kudharau alama zilizopo kwenye vivuko ili kuepusha ajali.

Katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Zakaria Mwansasu, Dk Burian ameviagiza vyombo vya dola mkoani humo kuwachukulia hatua za kisheria madereva wasizingatia kanuni za usalama, hasa inayoelekeza tahadhari kwenye vivuko vya reli.