Watu 14 wafa ajali ya gari Simiyu

Muktasari:

Watu 14 wamefariki dunia baada ya gari ya waandishi wa habari iliyokuwa kwenye msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RC), Robert Gabriel kugongana na gari ya abiria Hiace katika eneo la Nyamikoma wilaya ya Busega Mkoani Simiyu.

Mwanza. Watu 14 wamefariki dunia baada ya gari la waandishi wa habari iliyokuwa kwenye msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RC), Robert Gabriel kugongana na gari ya abiria aina ya Toyota Hiace  katika eneo la Nyamikoma wilaya ya Busega Mkoani Simiyu.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu akiwa eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Busega (DC), Gabriel Zakaria amethibitisha kutokea vifo hivyo.

Amesema kati ya vifo hivyo kuna vifo vya waandishi wa habari wanne na dereva wa waandishi na watu wengine sita walifariki papo hapo

Tamko la RC MWANZA baada ya AJALI ya Waandishi wa habari SIMIYU

“Ni kweli ajali hiyo imetokea, watu 11 wamefariki kwenye eneo la tukio wakiwemo waandishi wa habari wanne na dereva na wengine sita waliokuwa kwenye gari lingine” amesema Zakaria na kuongeza

“Dakika chache majeruhi waliopelekwa kwenye kituo cha afya cha Nasa watatu walifariki, wakiwemo wale waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara”  amesema

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyo, Blasius Chatanda amesema yupo katika hospitali ambako majeruhi walikopelekwa akiahidi kuwa atatoa taarifa baadaye.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel naye amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema yuko njiani kuelekea eneo la tukio.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi