Watu 19 waliwa na mamba, 20 wajeruhiwa Sengerema

Muktasari:

  • Utamaduni wa kuoga ziwani watajwa kuchangia watu kushambuliwa.

Sengerema. Watu 19 wamefariki dunia, huku 20 wakipata ulemavu wa kudumu kwa kushambuliwa na mamba katika Halmashauri ya Sengerema, mkoani Mwanza.

 Takwimu hizo zimetolewa jana Machi 2, 2024 na ofisa wanyamapori wa halmashauri hiyo, Paul Poncian alipozungumza na Mwananchi ofisini kwake.

Amesema matukio hayo yametokea katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kuanza mwaka 2019 hadi mwaka huu, huku utamaduni wa kuoga ziwani ukielezwa kuchangia watu kushambuliwa.

Poncian amesema wavuvi wanaofanya shughuli ndani ya Ziwa Victoria ndio waathiriwa wakuu wa kushambuliwa na mamba hasa wanaotumia vyombo visivyo rasmi katika uvuvi ‘madungudungu’ wanaochota maji na wanaooga ziwani.

“Matukio mengi hutokea kati ya Septemba na Januari, baada ya kufanya ufuatiliaji tumebaini ni kipindi ambacho mamba wanazaliana. Kwa hiyo unakuta mahitaji ya chakula kwao yanaongezeka ndiyo maana wanashambulia binadamu,” amesema Poncian.

Ametaja mikakati iliyopo kukabiliana na matukio ya wanyama hao kushambulia binadamu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) kuwa ni kutoa elimu kwa jamii inayozunguka ziwa kuchukua tahadhari wanapoingia au kufanya shughuli kando mwa ziwa.

“Wakazi wa Sengerema kwa asilimia zaidi ya 50 wanategemea shughuli za uvuvi au kilimo kando mwa ziwa kujipatia kipato, kwa hiyo hauwezi kuwatenganisha na Ziwa Victoria. Lakini tunawapatia elimu ya namna ya kuepuka mazingira hatarishi ya kushambuliwa na mamba,” amesema.

Ofisa Wanyamapori Msaidizi Daraja Kwanza wa Tawa wilayani Sengerema, Lolruck Mosses amesema mamlaka hiyo imekuwa ikifanya doria na misako ya mara kwa mara kuwauwa wanyama hao hasa waliotekeleza matukio ya kushambulia binadamu.

"Hivi sasa tumeanzisha kampeni ya utoaji elimu kwa wanafunzi shuleni, ili kuwajengea uwezo watambue wanapoenda ziwani wachukue tahadhari kwa sababu kule kuna viumbe wanaishi. Kwa hiyo, ni wajibu wa jamii kuchukua tahadhari wanapofanya shughuli kando mwa ziwa.

“Mkakati wa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ni kujenga vizimba katika maeneo ya wananchi kuwawezesha kuchota maji na kufanya shughuli zingine ziwani bila kushambuliwa,” amesema.

Vizimba hivyo amesema vimejengwa katika Kijiji cha Izindabo, Kata ya Lugata (Kome) na Kijiji cha Kanyala, Kata ya Bulyaheke.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Chifunfu, Denis Twilosaho amesema utamaduni wa wakazi wa wilaya hiyo uliozoeleka ni kuoga ziwani tofauti na nyumbani.

“Jamii yetu bado inaendeleza utamaduni wa zamani wa kuoga ziwani, bado hawajabadilika ndiyo maana ukifuatilia kwa kina utabaini matukio mengine yanatokea watu wakioga ziwani hasa usiku. Pia ukosefu wa vyanzo mbadala vya kupata maji unasababisha wakachote maji ziwani,” amesema Twilosaho.

Ameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya usambazaji wa majisafi na salama, uvuvi, na kutoa elimu kwa wananchi juu ya mbinu salama za kuendesha shughuli zao.

Pia kuweka sheria kali zinazodhibiti wananchi kufanya shughuli kando mwa ziwa kiholela jambo linalohatarisha maisha yao.

“Tunatambua watu wengine wanafanya mambo kwa mazoea, lakini kukiwa na vibao au sheria inayoonyesha kwamba hauruhusiwi kufanya shughuli yoyote katika eneo fulani lenye viashiria vya kuwepo wanyama hao hakuna mtu angeshambuliwa na mamba au kiboko,” amesema.

Simulizi walioathirika

Mkazi wa Kijiji cha Chifunfu kinachopakana na Ziwa Victoria, wilayani Sengerema, Nyandele Ernest, anaulaani utamaduni wa kuoga ziwani kutokana na kifo cha mkewe, Chilunda Bwire (34), aliyefariki dunia Februari 24, 2024 kwa kushambuliwa na mamba wakioga ziwani.

Shambulio hilo limemwachia kitendawili cha malezi kwa watoto watatu alioachiwa, akiapa kutorudia kuoga ziwani.

"Sitasahau, nilishuhudia mke wangu akiondoka baada ya kukwapuliwa na mamba, tuliishi kwa furaha na upendo, tukilea watoto wetu. Ningejua kwamba mke wangu yangemkuta haya nisingeruhusu tukaoge ziwani,” amesema Ernest.

Buhanza Ntulanalwo, mkazi wa kijiji hicho, anasema hatasahau alivyonusurika kifo baada ya kushambuliwa na mnyama huyo, akisalia kuwa na ulemavu wa kudumu baada ya mamba kuondoka na sehemu ya mkono wake.

“Wananchi wanaoishi kando mwa ziwa fanyeni kazi kwa umakini, uhai wako ni muhimu kuliko chochote kwa sababu kukosa umakini kwangu kumenisababishia nimekuwa na ulemavu wa kudumu wa mkono,” amesema.