Mume asimulia mkewe alivyoliwa na mamba akishuhudia

Muktasari:

  • Matukio ya watu kushambuliwa na mamba yamekuwa yakitokea mara kwa mara hivyo wananchi wameiomba Serikali kuhakikisha wanavuna mamba hao ili kuwapatia ahueni wananchi.

Sengerema. Mkazi wa kijiji cha Chifunfu kilichopo wilaya ya Sangerema mkoani Mwanza, Chindula Bwile (34) amefariki dunia baada ya kushambuliwa na mamba wakati akioga kwenye  Ziwa Victoria akiwa na mumewe.

Tukio hilo limetokea Februari 24, 2024 saa 2 usiku wakati Chindula akioga ziwani kabla ya kushambuliwa na mamba huyo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Chifunfu, Denis Dominic amesema familia hiyo inaishi kandokando ya Ziwa Victoria na wana utaratibu wa kuoga ziwani mara kwa mara.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akieleza kwamba Serikali imechukua hatua ya kumsaka mamba huyo.

“Kufuata tukio hilo, tayari idara ya wanyamapori wako eneo la tukio wakishirikiana na wananchi kumsaka mamba na mabaki ya mwili wa marehemu,” amesema mkuu huyo wa wilaya na kuongeza kuwa  marehemu ameacha mume na watoto watatu.

Kwa upande wake, Nyandele Ernest ambaye ni mume wa marehemu, amesema wakati tukio linatokea alikuwa na mke wake akimmulikia tochi akiwa anakoga.

Amesema alipozima tochi mamba huyo alifika na kumshambulia mke wake na kuondoka naye hadi sasa mabaki ya mwili wake hayajapatikana.

Mkuu wa kitengo cha usimamizi wa wanyamapori wilayani Sengerema, Paul Posian amesema tayari wako eneo la tukio wakishirikiana na wananchi kumsaka mamba huyo.