Mvuvi apoteza maisha akidaiwa kuliwa na mamba Mtera

Muktasari:

  • Mkazi wa Kijiji Cha Mtera, Kata ya Migoli, Mkoani Iringa, Hilary Ngatunga amefariki dunia baada ya kuvamiwa na mamba wakati akivua samaki katika Bwawa la Mtera.

Iringa. Mkazi wa Kijiji cha Mtera, Kata ya Kigoli Wilayani Iringa, Hilary Ngatunga amefariki dunia baada ya kuvamiwa na mamba wakati akivua samaki.

Hili ni tukio la pili kutokea katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja ambapo, Desemba mwaka Jana, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Chapuya, Kata ya Migoli alipoteza maisha baada ya kuliwa na mamba wakati akivua samaki kwenye bwawa hilo.

Diwani wa Kata ya Migoli, Benitho Kayugwa akizungumza na Mwananchi Digital leo, Januari 9, 2024 amesema ndani ya mwezi mmoja zaidi ya wavuvi wanne wanadaiwa kuuawa na mamba kwenye bwawa hilo.

Kayugwa amesema Ngatunga alijihimu kuvua samaki kama kawaida yake kwenye bwawa hilo lakini kabla hajatoka mamba alipiga mtumbwi na kumdaka.

"Hali sio shwari, wavuvi wanakadiria kila baada ya mita mbili kuna mamba. Kwa mwezi mmoja tumepoteza watu wanne, tunaomba mamlaka ziingilie Kati," amesema Kayugwa.

Baadhi ya wakazi wa katika eneo hilo, wamesema Mtera ndilo bwawa wanalotegemea kiuchumi hasa shughuli za uvuvi.

"Tunaomba mamba wavuliwe lakini pia kuna viboko ambao nao ni hatari tunaomba msaada wavunwe," amesema Kadri Mgeni, mmoja wavuvi hao.

Mhifadhi Mwandamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Asubuhi Kasuga amesema tayari wameomba kufanyika kwa utafiti kujua idadi ya wanyama waliopo ndani ya bwawa la Mtera ili wavunwe.