Watu 6,000 kutibiwa bure magonjwa ya macho

Wataalamu wa macho, Kumail Walji (kulia mbele) na Ally Khakoo wakimpima macho mmoja wa wazee waliofika katika kambi ya siku tatu ya matibabu ya ugonjwa huo, inaloendeshwa na taasisi ya kidini ya Bilal Muslim ikishirikiana na Better Charity ya Uingereza  na kampuni ya simu ya Tigo. Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

  • Watu hao  wanatarajia kupata elimu ya utunzaji, vipimo na matibabu ya macho  kupitia kambi ya siku tatu mkoani Mtwara

Mtwara. Zaidi ya wananchi 6,000 wanatarajia kupata elimu ya utunzaji wa, vipimo na matibabu ya macho bure kupitia kambi maalumu.

Hayo yameelezwa leo Aprili 27, 2024 na Mratibu wa kambi ya macho wa Taasisi ya Bilal Muslim Agency, Hassan Dinya katia kambi siku tatu ya macho wanayofanya kwa kushirikiana na Taasisi ya Better Charity ya Uingereza na kampuni ya simu ya Tigo.

Dinya amesema wanatarajia kuona zaidi ya wagonjwa 1,500 kwa siku, ambapo siku ya kwanza wagonjwa 20 walitakiwa kusafishwa macho.

 “Watu wengi hawana elimu sahihi juu ya utunzaji wa macho wanatumia boda wengine wanachomelea lakini hawajali juu ya umuhimu wa kutunza macho yao, hata wakati mwingine yakiwasha wanadharau na kuyaacha hilo lina leta athari kidogokidogo baadaye zinakuwa kubwa.”


“Ni hatari sana tuache kushika macho na mikoani bila kunawa na pia ukipata muwasho kwenye macho nenda hospitali upate huduma usipuuze,”amesema.


Naye Kaimu Mganga wa Manispaa ambaye pia ni Mratibu wa Huduma Tiba Manispaa wa Mtwara Mikindani, Dk Perensian Rwezaula amesema kuwa wananchi wengi kwenye eneo hilo wanakabiliwa na matatizo ya macho kutokana na mfumo wa maisha.

Amsema kuwa kupitia vituo vya afya vya manispaa wamekuwa wakipokea wagonjwa watano hadi 10 kwa siku  wanaofanyiwa  uchunguzi wa macho.

“Unajua mtindo wa maisha umekuwa ukichangia watu wengi kupata maradhi ya macho tumeanzisha kliniki kuboresha mtindo wa maisha ili kudhibiti magonjwa yanayoweza kusababisha magonjwa ya macho, ikiwemo shinikizo la juu la damu na kisukari,” amesema Rwezaula.

Naye Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Pwani, Aidan Komba amesema kuwa taasisi hiyo imetoa Sh350 milioni kwa ajili ya kuendeshea kambi hiyo na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ya macho.

“Huduma hii inatolewa bure ambapo tumedhamini kwa Sh350 milioni ili kuweza kupata huduma wananchi wote ikiwemo kupimwa, ushauri na miwani bure kabisa na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma,”amesema Komba.