Watu wasiojulikana wachoma gari la hakimu

Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Nyamilanda, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Emmanuel Jonathan lililoteketezwa kwa moto na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Mei 09, 2022.
Muktasari:
Gari hilo limeteketezwa usiku wa kuamkia Mei 09, 2022 wakati hakimu huyo akiwa amelala nyumbani kwake
Muleba. Watu wasiojulikana wameteketeza gari la Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Nyamilanda, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Emmanuel Jonathan.
Gari hilo aina ya Toyota Harrier limeteketezwa usiku wa kuamkia Mei 09, 2022 wakati hakimu huyo akiwa amelala nyumbani kwake.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Muleba, Toba Nguvila ameagiza Jeshi la Polisi wilayani humo kufanya uchunguzi ili kuwabaini watu waliofanya kitendo hicho.
"Ninaagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kuwabaini watu waliofanya tukio hilo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na kujichukulia sheria mkononi," amesema Nguvila.
Kwa upande wake Hakimu huyo amesema kuwa, siku ya tukio akiwa amelala usiku aliamshwa na vijana wa kazi kuwa gari linaungua moto ndipo aliamka na kuanza kuzima moto kwa kushirikiana na majirani ingawa gari lilikuwa limeshateketea.
Mkazi wa Nyamilanda, Terazias Anthon amesema kuwa, katika Kijiji hicho yamekuwa yakijitokeza matukio ya aina hiyo ya watu kujichukulia sheria mkononi.
Anthon ameviomba vyombo vya ulinzi kuwachukuliwe hatua watu waliofanya kitendo hicho ili iwe fundisho kwa watu wengine.