Watu wawili wafariki dunia katika matukio tofauti

Muktasari:

  • Watu wawili wamefariki dunia mkoani Kilimanjaro, katika matukio mawili tofauti.

  

Moshi. Watu wawili wamefariki dunia mkoani Kilimanjaro, katika matukio mawili tofauti.

Saumu Hassan (32) amefariki dunia baada ya kukanyagwa na Tembo akiwa shambani, huku mwingine ambaye bado hajafahamika, amefariki baada ya kupigwa na wananchi akituhumiwa kuiba pikipiki.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Juni 21, 2022 Kamanda wa polisi mkoani humo, Simon Maigwa amesema tukio la mwanamke kuuawa na Tembo lilitokea Juni 19, saa 12:00 asubuhi katika kitongoji cha kijiweni Kata ya Ngarenairobi wilayani Siha, wakati mama huyo akiwa shambani akichimba viazi.

"Mama huyu alikutwa amefariki dunia baada ya kujeruhiwa na Tembo, akiwa shambani anachimba viazi, ambapo alipata majeraha makubwa mwilini mwake, nitoe wito kwa wananchi kuchukua tahadhari pindi wanapokwenda shambani, hasa wale ambao wamepakana na hifadhi".

Kamanda Maigwa amesema tukio lingine limetokea Juni 18 saa 1:00 usiku, katika kijiji cha Roo Kata ya Romu wilayani Hai, ambapo mtu mmoja anayedaiwa kuwa jambazi aliuawa kwa kushambuliwa na wananchi.

Kamanda Maigwa ameeleza kuwa, siku ya tukio anadaiwa kumkodisha dereva bodaboda aitwaye Seleman Rashidi (30) mkazi wa kwa Sadala na walipofika njiani kijiji cha Roo ghafla marehemu alianza kumshambulia kwa kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na kisha kumpora pikipiki.

"Mhanga alipiga kelele kuomba msaada, ndipo wananchi walifika eneo hilo na kumshuhudia jambazi huyo akitoroka na pikipiki hiyo, walimfukuza na alipoona anakamatwa alijificha kwenye kichaka na kuanza kushambulia wananchi kwa mawe kwa kujihami asikamatwe"amesema Kamanda Maigwa.

Kamanda amesema dereva bodaboda aliyejeruhiwa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Hai na hali yake inaendelea vizuri, huku mwili wa marehemu ukiwa umehifadhiwa katika hospitali hiyo kusubiri utambuzi.