Watu wenye ulamavu waomba faraja na upendo

Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Morogoro (Morpc), Lilian Lucas mwenye miwani akimkadhi mkurugenzi wa kituo cha Erick Memorial Foundation, Josephine Bakhita mfuko wa sabuni ya unga baada ya waandishi wa habari wanawake kutoa msaada wa vifaa kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mkoani Morogoro. Picha na Juma Mtanda

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa kituo cha Erick Memorial Foundation mkoani Morogoro, Josephine Bakhita, amesema makundi hayo yanakosa upendo na faraja.

Morogoro. Watu wenye ulemavu wa akili na watoto na wenye mahitaji maalumu, wameiomba jamii kuwapa upendo na faraja.

Akizungumza na waandishi wa habari wanawake waliotembelea kituo cha Erick Memorial Foundation leo Alhamisim Machi 7, 2024 mkoani Morogoro, mkurugenzi wa kituo hicho, Josephine Bakhita amesema makundi hayo yametengwa na kukosa upendo wa jamii.

“Wageni wetu wanapokuja hapa kituoni, watoto wa kike wanapenda kuwakumbatia mwanaume katika salamu na watoto wa kiume watakwenda kuwakumbatia wanawake, ili kupata faraja na upendo kutoka kwao na hali hiyo ni kwa sababu watoto hawa wamekosa faraja na upendo. Pia wanakosa mahitaji muhimu kama vyakula, mavazi, elimu na huduma za afya,” amesema Bakhita.

Anjelina Robert (14), anayesoma kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Uwanja wa Taifa anayeishi katika ituo hicho, amesema wasichana katika kituo hicho wana uhitaji wa taulo za kike na vifaa vya shule.

“Tuna uhitaji wa taulo za kike kwa sisi wanafunzi, kwani wakati wa hedhi inakuwa tatizo kujisitiri. Pia tunahitaji vifaa vya shule na mahitaji mengine kiujumla,” amesema Anjelina.

Naye Katibu wa Chama cha Waandishi wa habari Mkoa wa Morogoro (Moropc), Lilian Lucas amesema wametembelea kituo hicho kutoa msaada wa vifaa vya kibinadamu na kuonyesha upendo na faraja kwa watoto na walezi wao.

Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Morogoro (Moropc), Thadei Hafigwa na baadhi ya wanachama wa chama hicho wakiwa wamebeba vyakula na vifaa kw ajili ya kutoa msaada katika kituo cha Erick Memorial Foundation kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. Picha na Juma Mtanda

Lilian amesema wametembelea kituo hicho kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kilele chake ni kesho, Machi 8 kwa kutoa msaada wa vyakula, nguo na viatu.

 “Tunatambua mchango wa hiki kituo na sisi kama waandishi wanawake tumejihamasisha wanawake kwa wanaume ndani ya Moropc na kupata nguo na vyakula ambavyo tunaamini vitasaidia kusukuma siku mbele,” amesema Lilian.