Watuhumiwa kesi kusambaza mtihani la saba wafikia 10

Muktasari:
Mwalimu Jacob Adagi na Joel Naome wameunganishwa na wenzao 10 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kusambaza mitihani ya Taifa ya darasa la saba kwa kutumia mitandao ya kijamii na Telegramu.
Dar es Salaam. Mwalimu Jacob Adagi na Joel Naome wameunganishwa na wenzao 10 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kusambaza mitihani ya Taifa ya darasa la saba kwa kutumia mitandao ya kijamii na Telegramu.
Oktoba 19, 2022 watu 10 wakiwemo walimu saba walifikishwa katika mahakama hiyo wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuvujisha mitihani na kutengeneza nyaraka za uongo.
Washtakiwa hao ni Jonson Ondieka (37), Elinanami Sarakikya (33), Joyce Nyanyakika (50), Llyoyd Mpande (32), Ronalda Odongo (31), Dorcas Muroso (50), Alcheraus Malinzi (47) na Raphael Innocent wote ni walimu pamoja na wafanyabiashara Patrick Chawana (42) na Theresia Chitanda (37).
Wakili wa Serikali, Yusuph Aboud alidai mshtakiwa Adagi na Ngome wanakabiliwa na shtaka moja la kuvujisha mitihani ya Taifa ya darasa la saba ambapo wameunganishwa na wenzao 10 hivyo jumla ya washtakiwa wapo 12.
Aboud alidai kati ya Oktoba 11,2022 na Oktoba 12, 2022 sehemu isiyojulikana jijini Dar es Salaam washtakiwa hao na wenzao 10 ambao hawapo mahakamani hapo walisambaza mitihani ya Taifa ya darasa la saba kwa kupitia mitandao ya kijamii na Telegramu kwa watu wasiohusika.
Alidai upelelezi bado haujakamilika aliiomba mahakama hiyo shauri hilo lipangwe Novemba 30, 2022 ili waje na washtakiwa wengine 10 ambao walishasomewa mashtaka hayo.
Hakimu Mkazi Mkuu, Pamela Mazengo dhamana ipo wazi washtakiwa wanatakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh5 milioni awe na vitambulisho vinavyotambulika.
Hata hivyo washtakiwa hao walikidhi vigezo hivyo na wapo nje Kwa dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 30, 2022 kwa ajili ya kutajwa.
Katika mashtaka mengine yanayomkabili mshtakiwa Malinzi inadaiwa kati ya Oktoba 2,2022 na Oktoba 12, 2022 sehemu isiyojulikana mshtakiwa huyo akiwa na nia ya kudanganya alitengeneza nyaraka za uongo wa mtihani wa somo la uraia la darasa la saba aliijifanya mtihani huo ni halali umeandaliwa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).
Inadaiwa tarehe hiyo sehemu isiyojulikana mshtakiwa Malinzi akiwa na nia ya kudanganya alitengeneza nyaraka za uongo wa mitihani wa somo la maarifa ya jamii wa darasa la saba uliijifanya mtihani huo ni halali wa Taifa umeandaliwa na Necta.