Prime
Watuhumiwa mauaji ya Mchina wadakwa
Muktasari:
- Raia wa China aliuawa na watu wanaodaiwa ni walinzi binafsi wa kiwanda hicho kilichopo Mabibo, jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Mei 16, 2026.
Siha. Jeshi la Polisi limewakamata watuhumiwa wawili wenyeji wa kata za Makiwaru na Orkolili, Wilaya ya Siha, Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za mauaji ya mfanyabiashara na mmiliki wa kiwanda cha kuchakata chupa za plastiki cha XIL LI, Bhaozang Ge (50).
Mmiliki huyo raia wa China aliuawa na watu wanaodaiwa ni walinzi binafsi wa kiwanda hicho kilichopo Mabibo, jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Mei 16, 2026.
Baada ya tukio hilo, mwili wa Bhaozang Ge ulichomwa moto katika eneo maalumu la Makumbusho ya Dar es Salaam na majivu yake kuwekwa ndani ya kisanduku na kusafirishwa Mei 27, 2026 kwenda China kwa maziko.
Mwananchi imemtafuta Mkuu wa Wilaya ya Siha, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi wa wilaya hiyo, Dk Christopher Timbuka ambaye amethibitisha kukamatwa kwa watu wawili usiku wa kuamkia leo Jumapili Juni 7, 2026.
Amesema kwa taarifa zaidi atafutwe kamanda wa polisi mkoani humo.
"Wahusika wawili wamekamatwa usiku wa kuamkia leo Juni 7, 2026 na wale wengine wote waliokuwa wanashikiliwa wameachiliwa hivyo mtafuteni RPC kwa taarifa zaidi," amesema Dk Timbuka
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoani humo, Simon Maigwa ili kuthibitisha taarifa za kukamatwa kwa watuhumiwa hao, simu yake haikupokewa licha ya kupigwa mara kadhaa.
Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngaritati, Nuruel Kivuyo anakotoka mmoja wa watuhumiwa hao, amethibitisha kukatwa kwa watuhumiwa wawili.
Amesema wamekatwa wakiwa Nairobi, Kenya walikokimbilia kujificha.
Amesema kwa sasa watuhumiwa hao wapo kituo cha polisi na kwamba ndugu jamaa na marafiki waliokamatwa kwa upelelezi baada ya mawasiliano yao kufuatiliwa wakiwasiliana na watuhumiwa, wameachiwa baada ya kupatikana watuhumiwa hao.
"Ni kweli wamekamatwa wamasai wawili ambao walikuwa wanadaiwa kuhusika na mauaji ya Mchina na wamefikishwa kituo cha polisi," amesema Kivuyo.
Amesema taarifa zilizopo ni kwamba baada ya mauaji hayo kutokea watuhumiwa hao walikimbilia Tanga na baadaye walirudi nyumbani kwao Siha na baada ya kujua wanafuatiliwa walikimbilia Nairobi, Kenya.
Simulizi ya Mchina
Awali, Raia wa China, Bhaozang Ge, alikuwa anaishi ndani ya kiwanda cha XIL LI akiwa na mfanyakazi mwingine wa Kichina pamoja na walinzi.
Kiwanda hicho kinajihusisha na uchakataji wa plastiki na uzalishaji wa malighafi zinazotumika kutengenezea bidhaa mbalimbali za plastiki, huku kikiajiri mamia ya wafanyakazi.
Hata hivyo, Mei 19, 2026 mhasibu wa kampuni hiyo, Eversophy Michael alisema hakuna mfanyakazi aliyedhani siku hiyo ingeishia kwa kuuona mwili wa mwajiri wao ukiwa umetupwa mtaroni ndani ya kiwanda hicho.
“Tulifika asubuhi ya Jumamosi kama kawaida tukitegemea walinzi watufungulie geti, lakini tuligonga sana hakuna aliyekuwa anajibu, hapo ndipo hofu ilianza,” alisema Eversophy.
Alisema walijaribu kumpigia simu Bhaozang Ge mara kadhaa lakini simu yake haikupokewa jambo lililozidi kuwapa wasiwasi wafanyakazi waliokuwa wamekusanyika nje ya geti.
Eversophy alisema walimuita mfanyakazi mwingine wa Kichina aliyekuwa ndani ambaye hajui lugha ya Kiswahili vizuri ili awafungulie geti na walipoingia ndani walikuta hali ya ukimya mzito.
“Tulipoingia ndani tulikuta walinzi waliokuwa zamu usiku hawapo, lakini simu ya bosi ilikuwa ikiita ndani ya chumba chake hivyo tukapata wasiwasi na kuhisi kutakuwa na tatizo limejitokeza usiku,” alisema.
Alisema walipofungua chumba hicho walikuta simu ya Bhaozang Ge ikiwa ndani huku mwenyewe hayupo, hivyo walitoka nje ya kiwanda kwa ajili ya kuuliza walinzi wa geti lingine kama walimuona bosi wao akitoka.
“Hapo kila mtu alichanganyikiwa ndipo tulianza kuhisi kuna jambo baya limetokea usiku,” alisema Eversophy.
Kutokana na hali hiyo, alisema walianza kupiga simu katika vituo mbalimbali vya polisi wakidhani huenda kulikuwa na ugomvi uliosababisha baadhi ya watu kupelekwa kituoni, lakini hakuna taarifa iliyokuwa imepokelewa.
Katika hali ya sintofahamu, alisema walimuuliza mlinzi aliyekuwa kwenye geti kubwa ambaye aliwaeleza saa tisa usiku aliwaona walinzi wawili wa Kimasai wakiondoka, huku mmoja wao akiwa amebeba begi mgongoni.
“Walidai wanapelekana hospitali kwa sababu mmoja wao alikuwa anaumwa, kwa kuwa walikuwa walinzi wetu, hakuna aliyewashuku,” alisema.
Baada ya maelezo hayo, wafanyakazi walianza kuzunguka kila kona ya kiwanda hicho wakimtafuta mwajiri wao huku hofu ikizidi kuongezeka, kwani mmiliki huyo hakuwahi kutoka nje ya geti peke yake na bila sababu za msingi.
Alisema walikuwa wanatembea maeneo mbalimbali ya kiwanda hicho wakiwa na wasiwasi mkubwa, kila mmoja akiwa anaomba moyoni asikute jambo baya.
Lakini alisema safari yao iliishia kwenye simanzi kubwa baada ya kuufikia mtaro uliopo karibu na mashine za kusaga ndani ya kiwanda hicho.
“Tulipofika eneo la kuwashia mashine za kusaga malighafi ndipo tulikuta damu na mwili wa bosi wetu ukiwa kwenye mtaro, kila mtu alipigwa na butwaa watu walianza kulia, wengine wakashindwa hata kuzungumza,” alisema.