Watuhumiwa tisa wa ugaidi Arusha waachiwa

Muktasari:

  • Washitakiwa tisa wa makossa ya ugaidi wameachiwa huru na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, imewaachia huru watuhumiwa tisa waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka 26 ikiwemo mauaji, ugaidi na kujaribu kuuwa.

Walioachiwa huru ni Abdallah Labia, Ally Kidaanya, Abdallah Wambura, Rajab Ahmed, Hassan Said, Ally Jumanne, Yassin Sanga, Shaban Wawa na Ibrahim Herman.

Uamuzi wa kuachiwa huru kwa watuhumiwa hao tisa, umefanyika leo Jumatatu, Juni 19, 2023 na Jaji Agustino Rwizile aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo ya jinai namba 63/2022.

Hatua ya kuachiwa kwao, imetokana na kile kilichoelezwa na Jaji Rwizile kuwa ni baada ya mahakama hiyo kupitia ushahidi wa mashahidi 23 wa upande wa mashitaka.

Akisoma hukumu hiyo, amesema mahakama imejiridhisha kuwa washitakiwa wote tisa waliokuwa wanakabiliwa na makosa hayo hawana hatia, kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha makosa hayo pasipo na shaka.

Awali, washitakiwa hao walikamatwa na kushitakiwa kwa nyakati tofauti mwaka 2014, wakidaiwa kufanya mkutano wa kupanga mambo ya kigaidi, kutenda kosa la ugaidi kwa kutumia mali, kutengeneza bomu linalodaiwa kulipuka na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi kadhaa katika baa ya Arusha Night Park.

Juni 16, mwaka huu Mahakama hiyo iliwaachia huru watuhumiwa wengine 12 waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya ugaidi tangu mwaka 2014, ambapo kati yao, wengine tisa waliendelea kuswekwa mahabusu kutokana na kukabiliwa na mashauri mengine.

Katika sehemu ya uamuzi wa kesi hiyo, Jaji Rwizile ameeleza sehemu ya ushahidi wa washitakiwa nane kati ya tisa katika kesi hiyo, walidai kuwa walipigwa na kuteswa wakati wanaandika na kusaini maelezo ya uungamo polisi.