Watumishi afya matatani kwa tuhuma za wizi wa Sh520 milioni
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai ameagiza vyombo vya usalama mkoani humo kuwachukulia hatua kali watumishi sita wa afya wanaodaiwa kuhusika na wizi wa fedha Sh520 milioni za mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).
Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai ameagiza vyombo vya usalama mkoani humo kuwachukulia hatua kali watumishi sita wa afya wanaodaiwa kuhusika na wizi wa fedha Sh520 milioni za mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).
Kagaigai ametoa agizo hilo jana Jumatatu Julai 12, 2021 wakati walipokutana katika kikao kazi kilichohudhuriwa na Naibu Waziri wa Afya na wadau wa sekta ya afya mkoani humo.
Amesema ubadhirifu huo haukubaliki na kuwataka wote waliochukua fedha hizo kuzirejesha haraka iwezekanavyo.
"Huu Ubadhirifu umefanywa na watumishi wasio waaminifu wanaofanya kwenye taasisi zetu za afya na maduka ya kuuzia dawa, ubadhirifu huu haukubaliki, natoa maelekezo kwa vyombo vya usalama kuchukua hatua za haraka sana kuhakikisha fedha hizi zaidi ya Sh520milioni zinarejeshwa" amesema Kagaigai
Naye Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema watumishi hao wa afya wamekuwa wakishirikiana na maduka ya dawa kuandika dawa ambazo hazijatumika kwa wenye bima kinyume na taratibu kwa maslahi yao binafsi.
"Zipo baadhi ya hospitali wanashirikiana na watumishi wanachezea mfumo kwa kushirikiana na wenye maduka ,wanaingiza kwenye mfumo taarifa za wagonjwa wakiwemo manesi na Madaktari kisha wanachukua dawa kwa namna isivyo ,tumefuatilia na tumepata ushahidi wa namna walivyofanya kuanzia saa, tarehe na dakika ,"amesema Dk Mollel
"Tumekamata Watendaji ndani ya hospitali ya KCMC, Mawenzi na maduka ya dawa na tunaendelea kufuatilia hata kwenye ofisi zetu za bima ya afya kujua ni watendaji gani wanaoshirikiana na hizo hospitali,"amesema Dk Mollel