Watumishi kuomba uhamisho Rukwa kwamshtua RC Sendiga

Muktasari:

Mkoa wa Rukwa umepiga marufuku uhamisho wa watumishi kutoka mkoani humo kwenda mkoa mwingine ikielezwa kuwa ni hatua ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi iliyopo  sasa.


Sumbawanga. Mkoa wa Rukwa umepiga marufuku uhamisho wa watumishi kutoka mkoani humo kwenda mkoa mwingine ikielezwa kuwa ni hatua ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi iliyopo  sasa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,  Queen Sendiga ametoa kauli hiyo jana katika  kikao kazi maalumu cha wadau wa sekta ya elimu kilichofanyika shule ya sekondari  Sumbawanga.

Amesema mkoa una mahitaji makubwa ya watumishi wa kada za afya na elimu lakini jambo la kustaajabisha kila kukicha watumishi wachache waliopo nao wanaomba na kupewa  uhamisho.


"Tuliomba kazi na kuahidi tupo tayari kukaa eneo lolote Tanzania sasa kwanini watu wakipangwa Rukwa wakimbie," amesema.


Sendiga amesema atawasiliana na ofisi ya waziri mkuu na utumishi ili kisitolewe kibali cha  mtumishi yeyote kuhama kutoka mkoa huo kwa kuwa bado maeneo mengi kuna mahitaji ya watumishi hususani kada za afya na elimu.


"Zahanati ya Kirambo cha Mkorechi iliyopo mwambao wa Ziwa Tanganyika,  imefungwa kwa zaidi ya miezi nane sasa kwa kuwa haina wataalamu wa afya, hakuna daktari wala nesi....inawalazimu wajawazito wajifungulie nyumbani na wengine wanapoteza maisha.....nimeagiza ifunguliwe mara moja na huduma zitolewe," amesema.


"Pia kuna shule nimesikia ina mwalimu mmoja tu darasa la kwanza hadi la saba..., bado turuhusu uhamisho wa watu kwenda nje ya mkoa wakati sisi pia tuna mahitaji ya wataalamu haiwezekani."